Na Asha Mwakyonde, Dar es salaam
"NAKOSA mapromota wa ndani ya nchi wa kunipatia pambano la ngumi (Boxing),nachukuliwa kwenda kucheza nje, napenda kuchezea nyumbani. Hii ni kwa sababu mapromota wanahofu nitawatajia bei kubwa"haya ni maneno ya Bondia wa kike Halima Vunjabei.
Akizungumza na Ihojo Media juzi jijini Dar es salaam Halima ameeleza kuwa
changamoto inayomkabili ni kukosa mapromota wa Tanzania wa kumpatia mapambano na badala yake anachukuliwa kwenda kucheza nje ya nchi na kwamba hali hiyo inatokana na mapromota hao kuhofia kutajiwa bei kubwa ikiwa ni pamoja na kufanya upendeleo kwa bondioa wengine wa kike.
Bondia huyo ametaja sababu nyingine kuwa hapati mapambano ya ndani ya nchi kutokana na mapromota kuangalia watu wao ambapo kila mchezo wanacheza hao hai, hivyo anachukuliwa na watu wa nje kwenda kucheza.
"Napenda nicheze hapa nyumbani, Tanzania mimi ni nyumbani lakini naenda kucheza nje ya nchi sio kwa kupenda bali mapromota wa ngumi hawanipatii ridhiki nami nicheze hapa nchini na hii ni kwa kuhofia nitawatajia bei kubwa," amesema Halima.
Halima ameongeza sababu nyingine ya kutokupata mapambano ndani ya nchini ni kutokana na mabondia wenzake wa kike kumuogapa kucheza naye kila wanapogangiwa wanamkataa.
Kwa mjibu wa Halima madondia wa kike wapo zaidi ya 35 hapa nchini lakini hawajiamini wanapoingia kwenye pambano.
MATARAJIO YAKE
Halima ameongeza kuwa matarajio yake ni kufika mbali zaidi kupitia mchezo huo wa ngumi.
Amefafanua kuwa mchezo huo anauchukulia kama kazi nyingine wanazozifanya watu wengine ambayo inamuingizia kipato katika maisha yake.
MAHUSIANO
Akizungumzia mahusiano ya kimapenzi Halima ameeleza kuwa hana mahusiano ya kugandana gandana, hataki kumilikiwa anahitaji kummilika mwanaume.
"Sitaki kuwa na mahusiano ambayo hayataniweka huru, nahitaji mimi ndo nimmiliki mwanaume hata tukigombana nimwambie abebe kilicho chake aondoke, sitaki kwenda kwa mwanaume ambaye anakila kitu chake hii kwangu hapana," amesema.
WITO WAKE MABONDIA WA KIKE
Halima amewataka mabondia wa kike
wasiogope mchezo wa ngumi kwani ni kama ilivyo michezo mingine huku akiwashauri wasiogope kukomaa sura kama baadhi ya jamii inavyosema na kwamba hakuna ukweli wowote wa suala hilo.
Amesema mchezo wa ngumi ni mzuri na nipendwa hapa nchini ambao unashika nafasi ya pili ambapo nafasi ya kwanza ni mpira wa miguu unaopendwa na watu wengi.
"Mchezo wa ngumi ni mchezo ambao naupenda, nilianza kucheza mpira wa miguu lakini nikaona siendani nao ndio nikaingia kwenye ubondia nikafanya mazoezi nikaona mchezo huu naupenda," amesema Halima.
Halima amesema mchezo wa ngumi aliuanza tangu mwaka 2010 na kwamba mchezo huo anauchukulia Kama michezo mingine inavyotoa ajira kwa vijana.
0 Comments