WAZIRI UMMY: MATOKEO YA RIPOTI YA AWALI INAONESHA VIFO VYA WATOTO WACHANGA VIMEPUNGUA

 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

MATOKEO  Muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022 yanaonesha kumekuwa na ongezeko la watoto wanaozaliwa kwa kuhudumiwa na watoa huduma ya afya wenye ujuzi kutoka asilimia 66 mwaka 2015/16 hadi asilimia 85 mwaka 2022 (miaka 2 kabla ya Utafiti). 

Hayo yamesemwa jijini  Dodoma Leo Februari 7,2023 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizindua Ripoti ya 

ya awali ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Afya ya Uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria wa mwaka 2022  amesema 

mwenendo huo umekuwa na mchango mkubwa kwenye kupungua kwa vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5).

Waziri huyo amefafanua kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa mwaka 2022, kimefika vifo 43 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai ukilinganisha na vifo 67 kwa kila Watoto 1,000 waliozaliwa hai ilivyokuwa kwenye Utafiti kama huo uliofanyika mwaka 2015/2016. 

"Haya ni matokeo makubwa ya juhudi zinafanywa na Serikali katika utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea katika Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa ambao unalenga kupunguza vifo vya Watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi vifo 40 katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai ifikapo mwaka 2025/26," ameeleza.

Ameongeza kuwa  kasi iliyopo ya uboreshaji wa Sekta ya afya na sekta nyingine ambazo Serikali imeendelea kuwekeza kama kwenye sekta ya kilimo ambayo ina mchango mkubwa katika usalama wa chakula, kipato, afya na ustawi wa mwananchi, Tanzania itafikia lengo la vifo 25 vya watoto chini ya miaka mitano kama ilivyobainishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ifikapo Mwaka 2030.


Kwa mujibu wa Waziri Ummy hiyo itachangiwa  na juhudi za Serikali za kuhakikisha utekelezaji wa BIMA ya afya kwa wote,ambapo kwa sasa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka, 2022 yanaonesha kuwa asilimia 6.2 ya Watanzania wote wana bima ya afya ya aina yoyote, wanawake wakiwa ni asilimia 6.3 ya wanawake wote na wanaume ni asilimia 6.1 ya wanaume wote.

Ameongeza kuwa matokeo haya Muhimu ya Utafiti yataiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita inayoogozwa na Mheshimiwa Dk.Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika mipango ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa hasa katika eneo la Afya ya Uzazi na Mtoto. 

"Tunafahamu kabisa katika ngazi ya Kitaifa matokeo haya yatasaidia kupima utekelezaji wa baadhi ya viashiria vya Sekta ya Afya vya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025,Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2021/22 hadi 2025/26 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26," amesema. 

Amesema kuwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa, matokeo ya Utafiti huo yatasaidia kutathmini utekelezaji wa Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2050,Dira ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2050, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya Mwaka 2063 na Ajenda ya Kimataifa ya Mwaka 2030 kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu. 


Waziri  huyo ameeleza kuwa matokeo ya Utafiti huo  watatupatia uelewa mpana wa changamoto ambazo Wananchi wanaendelea kuzipata katika Sekta ya Afya na kuwezesha kuweka mipango ya kimkakati ya kuboresha zaidi sekta ya afya nchni.  

"Kwa kuwa Utafiti huu ndio unaotupatia taarifa za kitakwimu kuhusu vifo vya utotoni napenda nianze na hali ilivyo duniani,Mwenendo wa vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano umekuwa ukipungua duniani ambapo kwa sasa vifo vimepungua kutoka vifo 93 mwaka 1990 hadi vifo 38 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 punguzo la asilimia 59 ," amesema.

Ameongeza kuwa vifo vya Watoto chini ya mwaka mmoja navyo vimepungua kutoka vifo 65 mwaka 1990 hadi vifo 28 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 sawa na  punguzo la asilimia 56. 

Waziri Ummy amefafanya kwa upande wa kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwezi mmoja vimepungua kutoka vifo 37 mwaka 1990 hadi vifo 18 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 sawa na punguzo la asilimia asilimia 51 kwa makadirio ya IGME (UN Inter-agency Group for Child Mortality Estimation).

Amesema Kwa  upande wa Afrika, nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha vifo vya Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano  ambapo kiwango hicho ni vifo 155 kwa kila vizazi hai 1,000, kiwango hicho ni kwa mujibu wa Utafiti wa DHS 1994/95 uliofanyika nchini humo na Nchi ya Senegali ndio yenye kiwango kidogo cha Vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano (5) kwa kuwa na vifo 37 mwaka 2019 kwa kila vizazi hai 1,000.

 "Takwimu zinaonesha kuwa katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa takwimu zinazotokana na tafiti zilizofanyika hivi karibuni, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano viko juu katika nchi ya Sudan Kusini ambapo kuna vifo 124 kwa kila vizazi hai 1,000 (DHS 1989-90) na viko chini sana katika nchi ya Rwanda ambapo kuna vifo 45 kwa kila vizazi hai 1,000 (DHS 2019-20).

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema wanafamu suala la afya mama na mtoto jinsi linavyopewa kiwapumbele katika serikali inayoongoza na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Tunashukuru Rais Samia wetu kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa salama," amesema Mkuu huyo wa mkoa.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Anne Makinda,amesema kuwa utafiti wa awali ni miongoni mwa tafiti muhimu ambayo inawapa fursa za kutathimini hali ya afya nchini.

Ameeleza kuwa afya bora ni msingi kwa kuweza Kupambana na maradhi mawili ya ujinga na umasikini.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS),Dk. Albina Chuwa amesema Tanzania ni miomono mwa nchi 93 duniani zinazofanya utafiti wa afya ya uzazi na watoto.

"Tupo hapa leo kwa mujibu wa sura namba 361 Takwimu ambayo inatuhitaji Utafiti huu wa afya ya uzazi na mtoto matokeo yake yaende yakatumike katika sera zetu za afya na sera nyingine zote ambazo  kuboresha afya," amesema.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI