Na Asha Mwakyonde
TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kiwango cha matumizi ya huduma za uzazi wa mpango katika nchi zilizoendelea ni asilimia 72 , huku Tanzania ikiwa kwenye kundi la nchi zinazoendelea ikiwa na asilimia 27 tu ya matumizi hayo.
Hata hivyo takwimu za umoja wa mataifa za mwaka 2022 ya Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani imetaja, Afrika ya Mashariki kuwa eneo linaloongoza katika ukuaji wa idadi ya watu barani Afrika ikiwa na watu zaidi ya milioni 457.
Katika kukabiliana na hali hiyo, WHO, pamoja na jamii ya umoja wa mataifa bado zimeendelea kusisitiza umuhimu wa uzazi wa mpango.
Akizungumzia matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango Daktari wa Magonjwa ya Binadamu kutoka Hospitali ya Marie Stopes iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Dk. Mashingo Lerise anaeleza kuwa wanaotumia vidonge hivyo kwa muda mrefu wametakiwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata njia na matumizi sahihi ya kupanga uzazi.
Anaeleza kuwa dawa za uzazi wa mpango hazisababishi kupata saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kama inavyodhaniwa na wanajamii bali ni matumizi yasiyo sahihi.
Anasema wanaofika hospitalini hapo kabla hawajaanza kutumia uzazi wa mpango lazima wajue historia ya mteja wao ikiwamo mfumo wa maisha yake.
"Lazima kuna maswali utaulizwa, mfumo wa maisha,magonjwa unayougua kuna tatizo lolote ulipata kufanya hivi ni kutaka kujua vitu ambavyo vinaweza kuwasaidia na kumpatia njia sahihi ya kupata huduma ya uzazi wa mpango," amesema.
Dk. Lerise ameongeza kuwa kuna baadhi watu wanatumia uzazi wa mpango kwa kuwa rafiki yake anatumia na yeye anatumia kwa kuona wanafanana maumbile.
Anasema kuzorota kwa kwa kinga ya mwili, mtu ambaye ana maambukizi ya virusi vya ukimwi na hatumii dawa ipasavyo virusi vya saratani vinapata nafasi na kwamba madhara yake ni kuzaliana kwa haraka.
Dk. Lerise pia anasema watu wanaopata mimba chini ya umri mdogo wa miaka 16 nao wapo kwenye hatari zaidi ya kupata saratani hiyo.
MATIBABU YAKE
Anasema matibabu yake ugonjwa huo ni kama yalivyo magonjwa mengine inategemeana hatua ya ugonjwa ulipofikia.
" Kuna chanjo ya kinga ambayo inamzuia mtu kupata saratani kwa hapa nchini chanjo hii ilotolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 na hutolewa bure, " anasema.
Daktari huyo anasema lengo ni kuwalinda mabinti hao ili wasipate saratani ya shingo ya mlango kizazi na kwamba matarajio ni baada ya miaka kadhaa tatizo hilo litakuwa limepotea kabisa.
TIBA
Anaongeza kuwa wanatumia tiba mgano ya gesi maalumu kugandisha chembe hai ambazo zinaweza kuonyesha dalili.
Daktari huyo anafafanua kuwa tiba hiyo wanaoipata ni wale wenye tabia ya kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na pia inafanya kazi vizuri kwa mtu mwenye dalili za awali kabisa.
Anasema tiba nyingine ni kufanyiwa upasuaji na kuondoa mfuko wa mimba na mirija ya uzazi pia natibabu ya tiba ya mionzi ambayo inafanya kazi vizuri.
"Mara nyingi matibabu haya ya mionzi huenda sambamba na matumizi ya ya dawa kali 'Chemo therapy' hizi ni dawa maalumu zinazotengenezwa kwa ajili ya kupambana na chembe hai," anasema Daktari huyo.
Pia anasema tiba Shufwa lengo lake kubwa ni kumsaidia mgonjwa aweze kuishi na ugonjwa wake lakini kumuondolea madhila na kuendelea na shughuli zake za kawaida.
Kwa mujibu wa Daktari huyo kinachofanyika kwenye tiba Shufwa ni kuangalia kama mgonjwa ana maambukizi nyemelezi.
ELIMU
Anasema ni jukumu lao watoa huduma za za afya pamoja na wanahabari kuwafikishia Watanzania ujumbe sahihi.
Dkt. Lerise anasema jamii ikipata taarifa zilizosahii itaweza kujiepusha na kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo kwani kuna mambo mengi yanayoongeoleka.
FIKRA POTOFU
Daktart huyo anabainisha kuwa wengi wao wakishaona amepata ugonjwa huu anadhani ndio mwisho wa uhai wake.
" Wanajamii wamekuwa wakipeana habari mbaya juu ya ugonjwa huu kuwa mtu akiupata ndio tiketi ya kifo lakini pia kupeana ushauri usiofaa wa kiimani badala ya kwenda hospitali anaenda kwenye maombi kanisani," anaeleza.
Anasema imani hiyo ndio inayosababisha wagonjwa wengi kufika hospitali kwa kuchelewa .
Kwa upande wake Hadija Athumani mkazi wa Nzuguni Dodoma anaeleza kuwa tangu aanze kutumia dawa za uzazi wa mpango ni miaka mitatu sasa hajawahi kupata headhi.
"Nilochoma sindano ya kuzuia mimba huu ni mwaka wa tatu sijapata hedhi na nina wasi wasi hanaweza kupata madhara," anasema.
Naye Agnes John mkazi wa Mkonze anasema anatumia vidoge vya mpango wa uzazi ambapo vilimsababishia kupata ujauzi kabla ya muda ambao alipanga kupata mtoto.
0 Comments