INADES YAWAKUTANISHA WAKULIMA,WADAU WA MBEGU ZA ASILI KUJADILI NJIA BORA KUENDELEZA MAZAO YA ASILI


Na Asha Mwakyonde, Kondoa

KASI ya mabadiliko ya tabia nchi imetajwa kuleta tishio kubwa kwa mbegu za asili ambazo ndiyo hazina ya nchi sasa na vizazi vijavyo na kwamba endapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa mbegu hizo hasa zile zinazostahimili ukame zitapotea na kusababisha janga la kukosa uhuru wa kula kile kinachoweza kuzalishwa katika mazingira husika.

Hayo yamesemwa leo Disemba 12 na  Afisa Tarafa ya Kolo kwa niaba ya ofisi  ya Wilaya ya Kondoa Fred Bagule wakati akifungua kongamano la  wakulima na wadau wa mbegu za asili lililoandaliwa na Shirika lisilo na kiserikali la Inades-Formation Tanzania ambalo limefanyika katika Wilaya ya Kondoa amesema kuwa mbegu za asili ni utajiri wa thamani kubwa sio tu kwa kilimo  bali kwa mustakabali wa chakula.

Ameeleza kuwa uhakika wa chakula huwezesha kuwa na taifa huru linaloweza kujilisha lenyewe bila kuwa tegemezi kwa vyanzo vya mbegu kutoka  nje ya nchi.

"Kongamano hili la siku mbili lenye kaulimbiu isemayo “Preserving Local Seeds for Food Sovereignty,” au “Utunzaji wa mbegu za asili kwa uhakika na uhuru wa chakula linalenga kutoa  fursa nzuri ya kubadilishana mawazo na mbegu, kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wengine, na kuweka mikakati endelevu ya kuhakikisha kwamba mbegu za asili hazipotei," amesema Bagule.

Afisa huyo aliongeza kuwa wanapopigania kuhifadhi mbegu hizo za asili, wanalinda utamaduni wao wa kilimo na kusaidia na  kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa chakula katika nyakati zote. 

Amesema kuwa wanahitaji kujenga uwezo wao wa ndani wa kuzalisha, kuhifadhi, na kutumia mbegu za asili ili kuweza kujitosheleza kwa chakula na kuepuka utegemezi usio wa lazima.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la nades-Formation Tanzania (IF TZ),
 Mbarwa Kivuyo amesema mchango wa mbegu za asili haujazingatiwa ipasavyo katika uandaaji wa sera mbali mbali ikiwemo Sheria ya Mbegu nchini ya mwaka 2003 na marekebisho yake.

 'Kupitia kongamano kama hili, hoja za wakulima na wadau wa mbegu zinaweza kufika katika meza za watunga sera," ameeleza Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi Mtendaji huyo Amefafanua kuwa kongamano hilo (ARF 2023) limeandaliwa kwa malengo kuwaleta pamoja wakulima na wadau wengine wa sekta ya mbegu kuonesha aina mbali mbali za mbegu za asili, kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya mbegu nchini kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu hatma ya mbegu zetu za asili hapa nchini Tanzania.

Amesema kuwa malengo mengine ni Kujadili masuala ya kisera yanayoweza kuchajisha ama kuathiri uhuru wa wakulima na jamii kurithishana na kubadilishana mbegu zao bila kuzuiwa na mtu yeyote, kutafuta njia bora zaidi ya kuendeleza mazao ya asili katikati ya janga la mabadiliko ya tabia nchi ulimwenguni.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI