UCSAF YAFADHILI WANAFUNZI WA KIKE MASOMO YA TEHAMA

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),umetoa ufadhili kwa wanafunzi wawili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),ambao wote wanasoma Shahada ya Sayansi ya uhandisi katika Maudhui ya Kidijitali na Utangazaji (Bachelor of Science in Digital Content and Broadcasting Engineering).

Ufadhili huo umelenga kuwawezesha wanafunzi wanaotoka katika familia zenye hali duni kiuchumi kuweza kusoma masomo ya sayansi katika eneo la mawasiliano.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo  Disemba 8, 2023 Mtendaji Mkuu wa mfuko huo Justina Mashiba katika hafla ya kusaini mkataba wa kufadhili wa wanafunzi hao alisema kuwa
mfuko huu umetoa shilingi 5,000,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka mmoja ambapo itatoa hadi watakapomaliza kusoma yao.

Mtendaji Mkuu huyo ameeleza kuwa gharama hizo ni pamoja na ada za chuo, gharama za malazi, gharama za chakula, bima, shajala (vitabu, madaftari, nk), gharama za elimu ya vitendo (field work), gharama za usajili na gharama nyinginezo.


 Amesema UCSAF imeingia makubaliano na vyuo hivyo ambayo yanalenga kuweka ushirikiano kwa taasisi hiyo kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kike wanaosoma shahada za sayansi katika eneo la mawasiliano ya simu, Posta na utangazaji. 

Amewataja wanafunzi  wa mwaka wa kwanza kutoka UDOM ambao wamesaini mkataba huo kwa niaba ya wanafunzi wengine kuwa ni Rebeca Mwakyembe na  Mariam Fweda 

"Kuna wengine wanne kutoka chuo cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST),na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), na tutawafadhili kulingana na ada za vyuo vyao," ameeleza.

Mtendaji huyo amefafanua kuwa
kwa mwaka wa fedha 2023/24, wanafunzi wa kike wanaofadhiliwa ni wale wanaosoma shahada za uhandisi katika masuala ya mawasiliano ya simu na utangazaji.

Ameongeza kuwa  maeneo hayo kwa muda mrefu yamekuwa yakihodhiwa na wanaume na kwamba ufadhili huo unakuja kuleta chachu kwa wanafunzi wa kike kupenda kusoma masomo yanayohusiana na uhandisi wa mawasiliano.

Kwa upande wake mwanafunzi Mwakyembe amesema kuwa atahakikisha anasoma kwa bidii na kupata ufaulu mzuri ili asifutiwe ufadhili kutokana na vigezo walivyopewa na kufikia malengo yake aliyojiwekea.

Naye Fweda amesema kuwa atajitahidi kufikisha moja ya vigezo vya ufadhili huo kwa kusoma na kupata alama ya GPA 3.5 pamoja na kutokuwa na tabia mbaya chuoni hapo.


Kaimu Makamu Mkuu  wa UDOM Dk. Florence Rashidi  amesema udhadhili huo utaenda kuleta mwanga kwa wanafunzi  hao ambapo utawasaidia kujisajili chuoni hapo.

"Wanafunzi hawa walikuwa bado hawajajisajili kuonesha kuwa walikuwa na uhitaji pia tunawashukuru UCSAF tumekuwa tukishirikiana katika maeneo mbalimbali hivyo tunaomba ushirikiano huu usiishie hapa tuendelee zaidi,"amesema.

UCSAF ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yenye jukumu kubwa la kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mijini yasiyo na huduma au yenye uhafifu wa huduma za mawasiliano.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI