TAFORI KUFANYA TATHIMINI YA RASILIMALI ZA MISITU KUONGEZA TIJA KATIKA VIWANDA VYA MAZAO


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania( TAFORI),itaendelea kufanya tathmini ya rasilimali za misitu kwa ajili ya kuongeza tija katika viwanda vya mazao ya misitu kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Mashariki na Kusini; kukamilisha tathmini ya mchango wa Sekta ya Misitu kwenye Pato la Taifa (GDP) kwa kutumia njia ya “green accounting”.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, leo Mei 31,2024 bungeni jijini Dodoma Waziri wa wizara hiyo, Angellah Kairuki amesema kuwa kazi nyingine zitakuwa kuendeleza tafiti za idadi ya miti, hali ya masoko, na mchango wa aina 3 za miti ya asili yenye fursa kubwa kibiashara, kufanya tafiti kwa kutumia teknolojia bora ya kuzalisha nishati mbadala; na kufanya utafiti wa kuangalia jinsi wadudu wachavushao wanavyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Kairuki ameeleza kuwa TAFORI itafanya tathmini ya ukuaji wa miti aina ya mianzi kwenye Mikoa ya Kanda ya Mashariki, Kusini-Mashariki na Nyanda za Juu Kusini, kufanya tathmini ya miti dawa na matumizi yake kwa ajili ya kuboresha maisha na uhifadhi wa misitu katika eneo la Milima ya Tao la Mashariki, kufanya utafiti wa faida na hasara ya biashara ya utomvu unaozalishwa kutoka kwenye miti katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Ziwa na kuchunguza athari za mizunguko ya uvunaji wa spishi za misindano na mikaratusi kwenye uzalishaji na ubora wa mbao.

"TAFORI itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi kwa kuwezesha watumishi 28 kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi 17 kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi," amesema Waziri huyo.

Amefafanua kuwa TAFORI itajenga jengo la Kituo cha Utafiti cha Tabora na kukamilisha ukarabati wa jengo la Kituo cha Utafiti cha Malya. 

Waziri Kairuki ameongeza kuwa Taasisi kwa kushirikiana na wadau wa nje na ndani ya nchi itaandaa Kongamano la 3 la Kimataifa la Sayansi linalotegemewa kukutanisha takriban wadau 500 wa ndani na nje ya nchi.

Amefafanua kuwa mada kuu katika Kongamano hilo ni "Urejeshaji wa Mandhari ya Misitu kwa Maendeleo Endelevu ili Kukabiliana na Mabadiliko ya TabiaNchi (Restoring Forest Landscapes for Sustainable Development and Climate Change Mitigation)".

Waziri Kairuki ameeleza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kufanyika tarehe 11-13 Disemba 11 Hadi 13 mwaka huu jijini Arusha.

Amesema Taasisi hiyo ina jukumu la kufanya na kuratibu tafiti za misitu na ufugaji nyuki na kutoa ushauri wa kitaalam katika nyanja za misitu na ufugaji nyuki. 

"Katika kutekeleza majukumu yake, Taasisi imefanya jumla ya tafiti 17 zikiwemo tafiti 5 za kimkakati. Tafiti za kimkakati zilizofanyika ni pamoja na tathmini ya 

rasilimali za misitu kwa ajili ya kuongeza tija katika viwanda vya mazao ya misitu Nchini," amesema.

Amebainisha kuwa tathmini hiyo imefanyika katika Mikoa ya Kanda za Magharibi, Kati, Nyanda za Juu Kusini na Ziwa ambapo imebainika 

kuwepo kwa viwanda takriban 940 vya msingi (viwanda vinavyopokea malighafi moja kwa moja kutoka msituni) vyenye mahitaji ya malighafi za mita za ujazo 7,473,826. 

Waziri hiyo amesema tathmini imebaini kuwa malighafi zinazopatikana kwa sasa ni mita za ujazo 3,772,239 sawa na asilimia 50 ya mahitaji na kwamba

tathmini ilibaini uwepo wa takriban hekta 266,457.98 zilizopandwa miti kwa ajili ya kutoa malighafi kwenye viwanda vya misitu vilivyopo nchini. 

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI