Mwanza
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma kanda ya ziwa imefungua mafunzo ya siku tano ya matumizi ya Mfumo wa NeST kwa watumishi wa taasisi nunuzi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa jana Mei 20, katika ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ambapo zaidi ya Washiriki 150 wamehudhuria.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Bi. Happiness Msanga amesema mafunzo haya yanaenda kunogesha chachu ya Serikali katika jitihada za kupata thamani halisi ya fedha katika Ununuzi wa Umma.
“Niwapongeze sana PPRA kwa namna wanavyowajibika kuendesha mafunzo haya, kwani mwishoni tunaamini baada ya muda kila mtumishi wa Umma atakuwa amepatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo suala ambalo litaleta chachu katika upatikanaji wa thamani halisi ya fedha. Alisema Bi Happiness.
Meneja wa Kanda ya ziwa wa PPRA Mhandisi Juma Mkobya ameongeza kwa kusema kuwa hatua hiyo ya utoaji mafunzo kwa kanda inaakisi nia njema ya PPRA na Serikali kwa ujumla kuhakikisha inazisogeza karibu huduma kwa wadau wake na jamii kwa ujumla kwa kadri inavyowezekana suala ambalo limechochea msukumo wa Uanzishwaji wa Ofisi za Kanda.
“ Kama inavyofahamika kuwa Serikali inajaribu kuangalia kila namna ya kuweza kuwapa huduma bora wanajamii, hususani raia wake kwa kuhakikisha inaweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa huduma na fursa wanazostahili” alisema.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni PPRA imeongeza ofisi 5 mpya za Kanda zinazoifanya Mamlaka kuwa na ofisi 6 za Kanda sambamba na Ofisi ya Makao Makuu iliyopo jijini Dodoma zinazojumuisha Ofisi ya Kanda ya Pwani iliyopo Dar es Salaam, ofisi ya kanda ya ziwa iliyopo Mwanza, Kanda ya Kati na Magharibi iliyopo Mkoa wa Tabora, kanda ya Kaskazini iliyopo Arusha, kanda ya Nyanda za juu kusini Mkoani Mbeya, na ofisi ya kanda ya Kusini iliyopo Mtwara.
Mafunzo hayo kwa upande wa Taasisi za Umma yatatumia siku 5 hadi ifikapo Mei 24, 2024 kabla ya kutamatishwa na mafuzuzo ya Wazabuni yatakayofanyika Mei 25, 2024 hapohapo jijini Mwanza.
0 Comments