Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) linatarajia kufanya jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma kwa lengo la kuendeleza ushirikiano baina ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wizara hiyo Mwanaidi Ali Khamis amesema jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika Septemba 4, 2024 hadi Septemba 6, 2024 huku mgeni Rasmi katika Jukwa hilo akitarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Amesema jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali lilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Septemba 30, 2021 akifuatiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Oktoba3 na 4 ,2022 na kuhitimishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango Oktoba 3 hadi 5, 2023.
“Jukwaa hilo limetanguliwa na majukwaa ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika ngazi za wilaya na mikoa,ambako yamefanyika majadiliano ya kubadilishana uzoefu kuhusu fursa na changamoto katika utekelezaji washughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali, mafunzo yakujengeana uwezo, utambuzi wa mashirika yaliyofanyavizuri na maazimio ya kushughulikia changamoto zilizoibuliwa na wadau mbalimbali,” amesema Khamis.
“Katika ngazi ya kitaifa, Septemba 4, 2024 yatafanyika mafunzo kwa wasajili wasaidizi na wajumbe wa NaCoNGO wa Mikoa, uzinduzi wa madawati ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika sekta binafsi na majadiliano ya pamoja na wadau wa sekta binafsi, mjadala kuhusu nafasi ya asasi zisizo za Serikali (NSAs) katika uboreshaji wa huduma za afya nchini Tanzania.
Khamis amesema vilevile kutakuwa na mafunzo kuhusu usimamizi wa miradi, uandishi wa maandiko dhana ya miradi, uandishi wa taarifa ya mfadhili na ufuatiliaji na tathmini, programu za huduma za kijamii kupitia dhana ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (MSLAC) katika eneo la Nkuhungu, Chamwino na Chang’ombe.
Aidha Septemba 5, 2024 itafanyika mijadala kuhusu fursa za ndani na nje ya nchi za ufadhili kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, mfumo wa kisera na wa uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, uzingatiaji wa misingi ya uwazi, uwajibikaji, uadilifu na utawala bora katika utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na mjadala kuhusu teknolojia na ubunifu kwa ajili ya ustawi wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
Sambamba na hayo Mhe. Khamis ametoa wito kwa wawakilishi wa wizara, idara na taasi za kisekta, wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wasajili wasaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali, wanufaika wa miradi na afua zinazotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani, pamoja na jamii kwa ujumla, kushiriki katika jukwaa hilo kwa mustakabali wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kwa upande wake mchechemuzi kutoka World Vision Easter Mongi amesema kampeni hiyo kwa kushirikiana na maendeleo ya jamii inategemea kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania ikiaziwa mikoa 16 ambapo World Vision inapatikana.
Amesema wanatumia fursa hiyo ili waweze kupata wadau wengi katika kufikia mikoa mengine ambayo World Vision haipo.
“Tunashirikiana na Wizara 5 tukiamini kabisa wadau wote waliopo katika mikoa ambayo sisi hatupo wataenda kufanya ambacho sisi tunakifanya, lakini kampeni hii itadumu kwa miaka mitatu ilizinduliwa sasahivi hivyo ndani ya shirika tunategemea tuwe na bajeti isiyopungua dola milioni 3 katika kutekeleza kampeni hii,”
Mongi ameongeza kuwa, “ Wadau tunaowategemea ni wote watakao kuwepo ukumbini na tuna amini wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali,taasisi binafsi watafanya kitu katika nyazifa zao ili kutokomeza utapiamlo Tanzania.”
0 Comments