Na Moreen Rojas, Dodoma
SERIKALI imesema itaendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kwani inatambua malengo yao yakuweza kuwahudumia watanzania.
Hayo yameelezwa leo Septemba 6,2024 na Mhe.Dk.Doto Mashaka Biteko Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wakati akifunga jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali 2024 katika ukumbi wa jakaya kikwete jijini Dodoma.
Aidha ameongeza kuwa mashirika hayo yahakikishe hayaharibu utamaduni wa kitanzania kwani hakuna mtu yeyote ambaye yuko tayari kuona mashirika haya yanaenda tofauti na tamaduni za kitanzania hivyo serikali imewaamini na wao wanapaswa kulinda imani hiyo kwa watanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalum Dk.Dorothy Gwajima amesema mashirika hayo yamekuwa yakishirikiana na serikali na Wizara yake itaendelea kushirikiana na NGO's ili kuweza kuhakikisha wanawafikia wananchi wenye uhitaji.
"Leo itazinduliwa Kampeni ya Kutokomeza Utapiamlo kwa Watoto ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26"
"Mpango huo umetoa mwongozo kwa wadau wa lishe juu ya utekelezaji wa afua zinazolenga kutatua changamoto za lishe duni zinazoathiri watu wa rika zote nchini"
Aidha ameongeza kuwa Kupitia uchambuzi wa taarifa za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 1,368 imebainika kuwa, jumla ya Shilingi trilioni 2.6 zilipokelewa na Mashirika hayo na kiasi cha Shilingi trilioni 2.4 kilitumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika nyanja mbalimbali.
Naye Rosemary Senyamule Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amempongeza Dkt. Biteko kwa kuendeleza maono ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia.
"Mimi ni chimbuko la NGO's na nafurahia namna ambavyo mmeweza kunilea hadi kufikia hapa kutoka kuwa Mkuu wa wilaya hadi Mkuu wa mkoa haya ni malezi yenu bora na yaliyotukuka asanteni sana kwa malezi yenu najivunia kutokea huko" Amesema Senyamule
Mwenyekiti wa Bodi ya mashirika yasiyo yakiserikali Najat Mwantumu Mahiza amesema madhumuni yao ni kupata kizazi cha watanzania walio bora kwa manufaa ya kizazi kijacho.
"Natoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kufanya kazi pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo yana mchango mkubwa katika kusaidia jamii"
"Natoa shukrani kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa ushirikiano wao kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hasa kati uchaguzi wa Baraza la Mashirika hayo. Naomba Baraza hili lipewe ushirikiano kwani wana dhamana kubwa kwa mustakabali wa nchi yetu" ameongeza.
Sanjari na hayo Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO), Jasper Lazaro Makala amesema Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini imeendelea kukua na kuimarika sio tu kwa idadi ya Mashirika yaliyosajiliwa bali kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali.
"Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya NGOs na Wizara nyingine za Kisekta kwa kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia uratibu wa Mashirika haya na Sheria nyingine za nchi", amesema.
Aidha ameongeza mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali hasa katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kauli mbiu ya jukwaa hilo ni "Mashirika yasiyo ya kiserikali ni wadau muhimu,washirikishwe kuimarisha utawala Bora".
0 Comments