Na Asha Mwakyonde, Dodoma
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imelaani Mauaji ya Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Ally Kibao aliyeuawa na watu wasiojulikana na kutupwa eneo la Ununio Jijini Dar es salaam.
THBUB imetoa pole kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Ally Kibao kwa msiba mzito wa kumpoteza mpendwa wao na kuwawaasa wananchi wote kuwa watulivu na wenye subira hasa katika kipindi hiki ambacho vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Hayo yamesemwa leo Septemba 9, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa tamko la kulaani mauaji mjumbe huyo wa Chadema ameeleza kuwa tukio hilo limetokea wakati THBUB inaendelea na kazi ya kufuatilia matukio kama haya yanayoendelea nchini.
Jaji Mstaafu huyo ameeleza kuwa THBUB inatambua maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa vyombo vya uchunguzi kufuatilia na kuwasilisha taarifa za kina kuhusu tukio hilo la kikatili na mengine ya namna hiyo yanayoendelea kutokea nchini
Amesema kuwa Septemba 7, 2024 zilipatikana taarifa kuhusu kupatikana kwa mwili wa Ally Kibao katika eneo la Ununio Jijini Dar es salaam.
Jaji Mstaafu huyo amefafanua kuwa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zinasema kuwa tarehe 6 Septemba, 2024 majira ya saa 12 jioni Ally Kibao, akiwa safarini katika basi la Tashrif lenye Namba za usajiri T 343 EES lililokuwa linatoka Dar es salaam kuelekea Jijini Tanga alichukuliwa na kushushwa na watu wasiojulikana wakiwa na silaha pamoja na pingu baada ya magari mawili aina ya Toyota Landcruiser Hardtop yasiyokuwa na namba za usajili kuzuia basi hilo katika eneo la Kibo Complex Tegeta ambapo watu wawili waliingia ndani ya gari na kumfunga pingu kisha kumshusha na kuondoka naye kwenda kusikojulikana.
"Taarifa hizi zilithibitishwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika alipokuwa akiongea na Vyombo vya Habari Jijini Dar es salaam kuwa mwili wa Ally Kibao umekutwa ukiwa na majeraha makubwa usoni, tunalaani Mauaji haya," ameeleza
Ameongeza kuwaatukio kama hayo yanarudisha nyuma jitihada za Serikali ya kuimarisha ulinzi, amani na usalama wa raia na mali zao nchini.
Hata hivyo amesema kuwa THBUB inatamka kuwa tukio hilo la utekaji na mauaji ni ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ambapo inalaani vikali vitendo hivyo.
Amesema ukatili dhidi ya binadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya mwaka 1977 huku akisema Ukiukwaji wa haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 15(1)(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
"Ukiukwaji wa haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuishi katika sehemu yoyote kama mtu huru kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 17(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ukiukwaji wa msingi wa utawala bora hususan utawala wa Sheria.
Ameeleza kuwa tume inaendelea na kazi ya uchunguzi kwa matukio mengine ya namna hii, ikiwa na pamoja na hili na itatoa taarifa yake kwa umma na kwamba inatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa THBUB na vyombo vingine vya dola vinavyochunguza tukio hilo.
0 Comments