WANANCHI TUMIENI SIKU SITA ZILIZOSALIA KUSALIMISHA SILAHA HARAMU KWA HIARI : ACP MADEMBWE

Na Mwandishi Wetu,  Dodoma. 

JESHI la polisi Mkoa wa Dodoma limewataka wananchi wote kutumia fursa iliyotolewa na Serikali kusalimisha silaha haramu kwa hiari ndani ya muda uliowekwa kabla ya Oktoba 31,2024 ambapo itakuwa tamati.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 25,2024 Jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi Kitengo cha udhibiti na usajili wa silaha makao makuu ya polisi Dodoma ACP Sébastian Madembwe, wakati akizungumza na Jambo FM ofisini kwake kuhusiana na zoezi hilo namna linavyoendelea.

"Wananchi watumie hii fursa iliyotolewa na Serikali kusalimisha silaha haramu wanazomiliki kinyume na sheria na endapo una taarifa za ndugu yako anamiliki silaha mwambie aweze kutumia fursa hii kuisalimisha kwani muda utakapokuwa umetamatika tutafanya ukaguzi na watakao bainika watachukuliwa hatua,"amesema. 

ACP Madembwe ameongeza kuwa hakuna changamoto yoyote iliyotokea katika zoezi hilo linaloendelea kwasasa kwasababu wamejipanga kupitia vyombo vya habari na polisi kata waliopo katika maeneo ambayo havifikii kuendelea kutoa elimu kuhusiana na zoezi hilo, hivyo ikitokea mtu hajasalimisha silaha yake atakuwa amefanya ukaidi.

Aidha amegusia kuhusu suala la watu kushindwa kuhifadhi silaha sehemu salama na kupelekea kuangukia katika mikono ya mtu asiye husika amesema hatua kari za kisheria zinachukuliwa dhidi yao. 

"Mmiliki yeyote ambaye atashindwa kuhifadhi silaha yake katika sehemu salama kiasi kwamba anatengeneza mazingira ya silaha hiyo kuangukia katika mikono ya mtu asiyehusika atakuwa ametenda kosa,"amesema. 

Hivyo amesema kuwa ni kosa la jinai kwa mmiliki yeyote wa silaha anayeshindwa kuitunza silaha yake katika sehemu salama na kutoa mfano kuwa unakuta mtu anaenda supermarket anaacha silaha kwenye gari na kupelekea waharifu kuvunja kioo cha gari na kuibiwa silaha hiyo, hivyo mmiliki atashtakiwa na kupelekwa mahakamani pamoja na kufutiwa leseni ya umiliki.

Pia ametoa wito kwa wananchi kutumia muda uliosalia wa siku Sita wa kusalimisha silaha haramu wanazozimiliki na sehemu za kusalimisha ni katika vituo vya polisi, ofisi za Serikali za Mitaa na ofisi za mtendaji kata na muda wa usalimishaji ni kuazia saa Mbili asubuhi mpaka saa Kumi jioni.

Zoezi la usalimishaji wa silaha ufanyika kila mwaka kuanzia mwezi wa Tisa na Kumi ambapo kwa mujibu wa takwimu za jeshi la polisi jumla ya silaha 337 zilisalimishwa mwaka jana pamoja na risasi 660.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU