HALMASHAURI YA MJI KONDOA ILIVYOTEKELEZA ILANI YA CCM KATIKA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI

Na Asha Mwakyonde DODOMA 

KATIKA kutekeleza makelezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 -2025 kupitia sekta mbalimbali Halmashauri ya Mji Kondoa iliyojiwekea malengo makuu kumi na moja, baadhi ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kufikia asilimia 100 ambapo kufikia Juni, 2024 imefikia asilimia 99 ya mapato yote.

Halmashauri ya Mji Kondoa ina eneo la hekta 130,591.11 zinazofaa kwa kilimo ambapo hadi sasa ni hekta 78,354.67 ndio zinatumika kwa ajili ya kilimo sawa na asilimia 60 kwa mujibu wa takwimu za Daftari la kilimo kwa Msimu wa 2023/2024. 

Pia Halmashauri hiyo ina kiasi cha hekta 450 ambazo zifaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kwamba bado hazijaendelezwa kutokana na kutokuwa na miundombinu.

Aidha kiasi cha hekta 8 zinatumika kwa umwagiliaji wa asili kandokando ya Mto Bubu na maeneo mengine madogomadogo katika Kata ya Kilimani Mtaa wa Damai na Kwantisi. 

Akizungumzia Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kupitia taarifa ya baraza la madiwani la mwisho wa mwaka 2023/2024,Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Kondoa Said Majaliwa anasema kuwa Halmashauri hiyo imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ushiriki wa maonesho ya nanenane Nzuguni Dododma ambapo Wataalamu 6 na wakulima na wafugaji 18 wamewezeshwa kushiriki maonesho hayo Agosti mwak huu. 

Anaeleza kuwa Halmashauri hiyo pia imewezesha usajili wa wakulima kwenye daftari la kilimo kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ambapo wakulima 4,373 wamesajiliwa kwenye madaftari hilo na kupandishwa kwenye mfumo. 

"Ili kumwezesha mkulima kulima kwa tija kwa kutumia mbolea Halmashauri imeweza kupokea jumla ya Tani 64 ambapo Tani 49 mbolea ni ya kukuzia na Tani 15 mbolea ya kupandia ambayo imeuzwa kwa wakulima kwa bei ya ruzuku," anasema mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo anaongeza kuwa Halmashauri hiyo imewezesha uchukuaji wa sampuli ya udongo kwa wakulima na kupima afya ya udongo ambapo jumla ya Sampuli za udongo 222 zimechukuliwa kwa wakulima na Taasisi na kupimwa afya ya udongo.


KINGA NA TIBA NA ELIMU KWA MIFUGO 

Akizungumzia utoaji wa kinga na tiba kwa mifugo ya aina mbali mbali, Majaliwa anafafanua kuwa 

jumla ya Kuku 31,276 wamepata Kinga ya Kideri, Ndui na Gumboro, Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo 10,310 wamepata chanjo ya Kimeta pamoja na Kinga ya Kichaa cha Mbwa 639 imetolewa. 

Mbali na utoaji kinga na tiba mkurugenzi huyo anasema kuwa wametoa elimu na ushauri kwa wafugaji na wakulima 12,464 ambapo wamepata elimu na ushauri juu ya kanuni bora za ufugaji wa kisasa pamoja na 

uogeshaji wa mifugo kwa kutumia njia ya mtumbukio na kunyunyizia jumla ya Mifugo 22,877 imepata huduma hiyo.

KUSIMAMIA MINADA

Anaeleza kuwa Halmashauri ya Mji Kondoa imesimamia uendeshaji wa minada ya awali inayofanyika na kwamba jumla ya Mifugo 3,135 iliuzwa, kati ya mifugo 4,345 iliyoingia katika mnada wa Bicha, Kolo, Iyoli na Serya.

Aidha anasema kuwa wamesimamia ukaguzi wa Mnyama kabla na baada ya kuchinjwa katika maeneo yaliyoidhinishwa ambapo jumla ya Mifugo 4,057 imechinjwa na kukaguliwa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeendelea kukusanya mapato kupitia vyanzo vyake kwa Mwaka 2023/2024 ambapo zaidi ya Shilingi milioni 283 imekusanywa hadi kufikia Juni 30, mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU