VIPAUMBELE VITANO VYA WIZARA YA ELIMU KWA BAJETI YA 2025-2026 HIVI HAPA

Na Asha Mwakyonde,DODOMA  

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara hiyo imepanga kutekeleza vipaumbele vitano katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Hayo ameyasema bungeni leo Mei 12,2025 jijini hapa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa Wizara hiyo alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo.

Ameeleza vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu, na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.

"Katika hili, juhudi zaidi zitatumika kupeleka vijana wa Kitanzania kusomea mambo ya sayansi ya nyuklia, mambo ya kompyuta na akili-unde kwenye vyuo bora vilivyo nje ya nchi," amesema Prof. Mkenda.

Akizungumzia taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Taifa ya UNESCO amesema Serikali kupitia Tume hiyo imeendelea kuratibu, kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mikataba na makubaliano ya kimataifa kwa kutekeleza majukumu hayo mbalimbali.

Waziri huyo ameeleza kuwa UNESCO imeratibu uanzishaji wa Kamati ya Kitaifa ya Kumbukumbu za Urithi wa Nyaraka wa Dunia itakayosimamia uingizaji wa kumbukumbu za nyaraka za Tanzania katika mfumo wa kidijiti wa Kumbukumbu za Urithi wa Dunia

"Tume hiyo imetoa elimu kuhusu umuhimu wa hifadhi hai pamoja na kuheshimu mipaka kati ya vijiji na hifadhi kwa Wananchi wanaoishi maeneo yanayopakana na Hifadhi Hai za Mazingira ambazo ni Jozan Chwaka Bay na Ziwa Manyara," alisema Waziri Mkenda.

Ameongeza kuwa UNESCO imeratibu mafunzo kwa vikosi vya ulinzi vinavyoshiriki operesheni za ulinzi wa amani katika mataifa mbalimbali kwa lengo la kulinda nyara za kiutamaduni katika kipindi cha majanga ya kivita na imetoa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya majukwaa ya habari katika kufikisha ama kupokea taarifa lengwa kwa waandishi na wadau wa habari 200 katika Mkoa wa Mwanza.




Post a Comment

0 Comments

WAZIRI MKUU MAJALIWA ACHAGIZA SIKU YA TANZANIA  MAONESHO YA  EXPO 2025, JAPAN