Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI ya Wanafunzi wa Chuo Kuu cha Dodoma (UDOSO), imezindua mfuko wa ufadhil wa masomo "UDOSO SCHOLARSHIP FUND" kupitia uwekezaji wa hati fungani katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT),ambapo umeekza shilingi milioni 100 wenye lengo la kuwasaidia wanafunzi wahitaji wa mwaka wa kwanza kwa kugharamia masomo yao.
Pia Taasisi zingine za elimu nchini kuiga mfano huu wa UDOSO wa kujenga mifumo imara ya kusaidia wanafunzi wao kwa kutumia ubunifu, ushirikiano na nidhamu ya matumizi ya rasilimali.
Hayo yamesemwa leo Juni 23,2025 jijini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo mara baada ya kuzindua mfuko huo amesema serikali ya Wanafunzi imeweza kuanzisha mfuko huu kwa kufanya uwekezaji wa kitaalamu kupitia ununuzi wa vipande (bonds), katika Benki Kuu ya Tanzania.
Prof.Nombo ameeleza kuwa faida iliyopatikana kutokana na uwekezaji huo sasa inakwenda kusaidia wanafunzi wahitaji wa mwaka wa kwanza kwa kugharamia masomo yao.
Amesema hilo ni jambo jipya la kibunifu, zuri, la kujivunia na kuigwa na vyuo na taasisi nyingine na kwamba uzinduzi huo unaashiria mafanikio makubwa na mfano bora wa uwajibikaji na ubunifu wa vijana wa Kitanzania katika kuwasaidia wenzao.
"Tunaishi katika kipindi ambacho changamoto za kiuchumi kwa wanafunzi zimeongezeka sana kiasi cha kupelekea baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo yao kwa kukosa ada na fedha za kujikimu, jambo hili linapoteza nguvu kazi ya Taifa na linakinzana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 toleo la 2023 inayolenga kuwa na watanzania walioelimika, " na kuongeza kuwa.
Kama mnavyofahamu, Serikali imekuwa ikigharimia kwa kiasi kikubwa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), " amesema Prof.Nombo.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Profesa Lughano Kusiluka amesema kuwa walishabgazwa na wazo la wanafunzi hao na kwamba waliliunga mkono kwa asilimia 100.
" Sijambo la kawaida serikali ya wanafunzi kufanya jambo kama hili tumezoeana kuona, kusikia viongozi wa wanafanzi wanagomba na kugawana fedha pindi wanapomaliza muda wao," amesema.
Awali rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho UDOSO Jackline Humbaro amesema kuwa mfuko huo utakuwa unafadhili wanafunzi 11 kwa mwaka huku faida itakayopatikana kupitia uwekezaji huo wa hati funguni ni shilingi milioni 15 kwa mwaka.
0 Comments