Na Asha Mwakyonde,Dodoma
MFUGAJI na mfanyabiashara wa njiwa wa mapambo kutoka Kampuni ya Fancypigeontz, Abdulaziz Almasi, amewahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa ya biashara ya njiwa, akieleza kuwa ni sekta inayochangia kipato kikubwa na ina soko pana nchini na kimataifa.
Akizungumza leo Agosti 6, 2025, katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea jijini Dodoma, Almasi amesema biashara ya njiwa bado haijachukuliwa kwa uzito unaostahili, licha ya kuwa na faida kubwa.
“Nimeleta aina 10 tofauti za njiwa wa mapambo katika maonesho haya, ambao bei zao zinaanzia shilingi laki nne hadi milioni moja kwa kila njiwa mmoja,” amesema.
Almasi amebainisha kuwa aina anazofuga kwa sasa zinatokea zaidi nchini Marekani, huku zingine zikitoka Ujerumani na maeneo mengine duniani. Alisisitiza kuwa njiwa wanaweza kufugwa kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo mapambo, nyama, au biashara ya kuzalisha.
Ameeleza kuwa chakula cha njiwa hao kinahusisha nafaka kama mtama, choroko na uwele, na kwamba njiwa ni wanyama wanaozaliana kwa haraka, hivyo kuwa chachu ya maendeleo ya mfugaji.
“Nimekuwa kwenye biashara hii kwa zaidi ya miaka 15. Nilianza na njiwa sita, leo hii ninamiliki zaidi ya njiwa 96 wa mapambo, mbali na wale wa kawaida,” amesema.
Hata hivyo, Almasi ametaja changamoto kubwa kuwa ni uelewa mdogo wa watu kuhusu thamani ya njiwa wa mapambo.
“Watu hushangaa bei, lakini hawajui kuwa kuna njiwa mmoja mwenye thamani ya hadi shilingi milioni moja. Wale wa ranging adieu na wa kifahari wana soko kubwa sana. Hii ni fursa halisi,” amesisitiza.
Amewakaribisha vijana na wafanyabiashara kuwekeza kwenye ufugaji wa njiwa, akisema ni njia mojawapo ya kuongeza kipato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.



0 Comments