TIRDO YAHIMIZA MATUMIZI YA MKAA WA MABAKI YA MAZAO KUTUNZA MAZINGIRA

Na Asha Mwakyonde,DODOMA 

SHIRIKA la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limewahimiza Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa miti, na badala yake watumie mkaa unaotokana na mabaki ya mazao mashambani ili kusaidia katika utunzaji wa mazingira.

Wito huo umetolewa leo, Agosti 6, 2025, jijini Dodoma na Mhandisi Paul Josephat Kimati kutoka TIRDO, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani humo.

Mhandisi Kimati amesema kuwa baada ya TIRDO kufanya utafiti kufuatia Agenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu nishati safi ya kupikia, walibuni njia ya kuzalisha mkaa kutokana na mabaki ya mazao mashambani.

“Tumefanya utafiti kwenye mabaki ya mazao mbalimbali kama vile vifuu vya nazi, vifuu vya chikichi, maranda ya mbao, mabaki ya mpunga na magunzi ya mahindi. Mabaki haya yanapochakatwa kwa teknolojia sahihi, yanazalisha mkaa bora unaoweza kutumika kama mbadala wa mkaa wa miti,” amesema Kimati.

Ameeleza kuwa mkaa huu una gharama nafuu na ni rafiki kwa mazingira, hivyo ni suluhisho endelevu kwa tatizo la ukataji miti unaochangiwa na uhitaji mkubwa wa mkaa wa kawaida.

Aidha, Mhandisi Kimati amewakaribisha wafanyabiashara na wananchi wanaopenda kujifunza kuhusu utengenezaji wa mkaa huo kufika ofisi za TIRDO ili waweze kupatiwa mafunzo.

“Huu ni mkaa wa kisasa, unaotokana na rasilimali tulizonazo mashambani. Tunawaalika wakulima na wananchi wote kutembelea banda letu hapa kwenye viwanja vya Nanenane ili wajifunze zaidi na kuona kwa vitendo kazi tunazofanya,” ameongeza.

Post a Comment

0 Comments

MASWI AKUTANA NA WAJUMBE WA AFRIKA WA UANGALIZI WA UCHAGUZI MKUU