DAKTARI: KULA CHAKULA KINGI KUPITA KIASI HUSABABISHA UGONJWA WA KISUKARI


Na Asha Mwakyonde

UGONJWA wa kisukari ni hali ya kuwa na kiwango kikubwa kwenye damu ambapo inagundulika pale mtu anapopimwa wingi wa sukuri na ni mojwapo ya magonjwa yasiyoambukiza.

Ugonjwa wa kisukari husababisha mishipa ya damu ishindwe kupeleka damu katika sehemu mbalimbali za mwili.

Akizungumzia ugonjwa huo katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, Daktari Mkaazi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Kitivo cha Afya, Dk Maseto Galikunga amesema zipo sababu ambazo zinachangia mtu kupata ugonjwa wa kisukari zikiwamo ulaji usiofaa na mtindo wa maisha.


ULAJI WA CHAKULA

Amesema kuwa katika tabia hatarishi ni pamoja na ulaji mbaya wa chakula kingi kupita kiasi (ulafi) na kwa mlo mmoja huchangia mtu kupata ugonjwa wa kisukari.

"Tabia nyingine hatarishi mtu anapokula vyakula vingi vyenye sukari kama keki, soda, juisi na vyakula vingine anapokula vyakula hivi anahatarisha afya yake," amesema Dk. Galikunga.

Amefafanua kuwa matumizi ya pombe na uvutaji wa sigara vinaharibu kongosho ambapo litashindwa kufanya kazi kwa kuwa ndio linatoa vichocheo vya Insulini ambayo inasaidia kwenye mmeng'enyu wa sukari na uhifadhi.

Dk. Galikunga amesema kongosho likiharibiwa litashindwa kutoa Insulini ambapo mtumiaji wa sigara na pombe sukari itakapo ingia kwenye damu itashindwa kuhifadhiwa kwenye seli na kutumika kwa matumizi mengine.

Ameongeza kwamba mtu kuwa na unene kupitiliza ni hatari  wataalamu wanangalia unene huo kwa kupima uzito na urefu wa mtu huyo .

" Kuna viashiria ambayo vitatuonesha kuwa huyu mtu unene wake umezidi na wakati mwingine tunawapima kiuno na hipsi ili kutafuta wastani na wastani huu ukiwa mkubwa tunajua ana unene wa kupitiliza," ameeleza.

DALILI ZA KISUKARI

Akizungumzia dalili za ugonjwa wa kisukari daktari huyo amesema kukojoa mara kwa mara ni moja ya dalili za ugonjwa huo huku akisema mtu anapoanza kuona dalili za kisukari tayari ameshakuwa na ugonjwa.

Dk. Galikunga amefafanua kuwa dalili nyingine  ni kunywa maji mengi, kusikia kiu mara kwa mara ,kuwa na hamu ya chakula pamoja na kula lakini bado anahitahi kula zaidi na  hiyo inatokana kwamba sukari haijaenda kwenye seli na kuweza kutumika kwenye shughuli mbalimbali za mwili na kujiona hana nguvu.

"Dalili nyingine hazipo wazi kwa ugonjwa wa lakini  mgonjwa anaweza kuwa na hali  ya kukosa nguvu na akipata madhara ya ugonjwa huu  anaweza akapata hali ya kuchanganyikiwa, maumivu ya tumbo, akasikia ganzi kwenye miguu na mikono, maumivu makali ya kifua na kupata kiharusi (Stroke)," ameeleza.


VIPIMO

Amebainisha kuwa wanaweza kumgundua mtu ana ugonjwa wa kisukari hata baada ya miezi mitatu iliyopita kwa kutumia
Kipimo cha Hemoglobini ya Glycosylated (HbA1c),ambacho kinaonesha alikuwa na ugonjwa huo kwa kipindi hicho.

Daktari huyo pia amesema kipimo hicho hutumika kama sehemu ya ufuatiliaji wa matibabu kwa mgonjwa kujua dawa anazotumia zinamsaidia au hazijamsaidia.

Amesema ugonjwa wa kisukari una mchango mkubwa kwenye magonjwa yasiyaambukiza kwa mujibu wa takwimu za Jarida la kimataifa la afya "The Lancet" ambapo zinaonesha takribani watu milioni 529 wana tatizo la ugonjwa huo na hapa nchini kati ya watu wazima asilimia 10.3 wanatatizo hilo.

MATIBABU  YAKE

Akizungumzia matibabu ya ugonjwa huo ameeleza kuwa yanapatikana sehemu mbalimbali nchini ikiwamo Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma na kwamba matibabu hayo yamegawanywa katika mara mbili ambayo ni ya kutumia sindano ya Insulini na vidonge vya kupunguza wingi wa sukari kwenye damu.

Daktari huyo amefafanua kuwa mgonjwa atatumia sindano kila siku na dawa hizo za kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu pia  atatumia kama ilivyo sindano.

Ameongeza kuwa kila mgonjwa ana matibabu yake kutokana na alivyo na kutegemea na unene alionao na kwamba dawa ambazo atatumia huku akisema wengine ni watu wazima hivyo matibabu yao yanatofautiana.

"Zipo dawa za aina mbalimbali za Insulini za kuchoma pia zitategemeana , dawa hazifanani zinategemea na uzito wa mtu na mgonjwa mmoja mmoja,"ameeleza.

Amefafanua kuwa wakati wa matibabu mgonjwa atatakiwa kupima sukari  kila asubuhi na jioni kabla ya kutumia dawa au sindano kwa ajili ya kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu.

WAGONJWA WANAOWAPOKEA

Amesema kuwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma wanawapata wagonjwa wa aina  mbalimbali ambao watawagundua wana ugonjwa huo wakiwa wamefika kupata matibabu ya magonjwa mengine.

"Katika ule upimaji wa kawaida wa siku zote tunagundua kuwa mgonjwa ana kisukari wakati amekuja na tatizo jingine  na kuna wengine wanakuja tayari wanadalili za ugonjwa wa kisukari, wengine wakiwa wameshapata madhara ya kisukari hivyo tunapokea wa aina zote .

Ameongeza kuwa kundi kubwa la wagonjwa wa kisukari wanaowapokea ni wale ambao tayari wameshapata madhara ya ugonjwa huo.

Dk. Galikunga amesema wanapata wagonjwa wa kisukari wa rika mbalimbali kuanzia watoto ambao huwa na aina ya kwanza ya ugonjwa huo na  kwamba wanawapata wa rika zote ingawa watu wazima ndio wengi.

Daktari huyo ametoa wito kwa Watanzania kujitahidi kuacha tabia hatari ambazo zinaweza kusababisha kupata ugonjwa wa kisukari ikiwamo ulaji mbovu wa chakula ikiwa ni pamoja na kula vyakula vingi kwa wakati mmoja,kula vyakula vya sukari kwa wingi,kupunguza unene kwa kufanya mazoezi, kuacha matumizi ya pombe na sigara.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU