MRADI WA RADA WATENGEWA BILIONI 15, UJENZI WA MAKAO MAKUU YA TMA KUANZA DODOMA

 
Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Mradi wa Rada, Vifaa na Miundombinu ya Hali ya Hewa kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),umetengewa jumla ya Shilingi bilioni 15.00 fedha za ndani ili kutekeleza kaza mbalimbali.

Akiwasilisha hutuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni leo Mei 6, 2024 Jijini Dodoma, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kukamilisha malipo ya uundaji wa Rada zitakazofungwa Dodoma na Kilimanjaro na ujenzi wa miundombinu ya Rada hizo.

Prof. Mbarawa amesema nyingine ni ununuzi wa vifaa vya hali ya hewa pamoja na mitambo ya mawasiliano, kuendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki pamoja na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami, kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya TMA Jijini Dodoma, ujenzi wa kituo kimoja cha hali ya hewa kilimo,ukarabati wa vituo viwili vya hali ya hewa.

Ameongeza kuwa kazi nyingine ni pamoja na jukamilisha malipopamoja na ufungaji wa vifaa vya uangazi katika Bahari ya Hindi vitakavyofungwa Zanzibar, Dar es Salaam na Bagamoyo, na kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato.

Akizungumzia huduma za hali ya hewa Prof. Mbarawa amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Mamlaka hiyo imeweka lengo la kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 15.98 kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na mapato yatokanayo na tozo za huduma za hali ya hewa, hususan zitumiwazo katika usafiri wa anga na majini. 

Waziri huyo ameeleza kazi zitakazotekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/25 ni kuboresha huduma za hali ya hewa kwa sekta mbalimbali zikiwemo: sekta za nishati, madini, rasilimali maji, usafiri, kilimo, utalii na ujenzi kuendelea kuimarisha udhibiti,na usimamizi wa ubora wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa sekta ya usafiri wa anga na shughuli zinazofanyika majini kulingana na vigezo vilivyopo.

"Kufanya tafiti za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi,kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kutumia huduma zinazotolewa na TMA,kudhibiti na kuratibu huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kwa kuhakikisha taratibu na matakwa ya kisheria yanafuatwa katika utoaji wa huduma hizi," ameeleza.

Amesema kuendesha na kuimarisha mtandao wa vituo vya hali ya hewa hapa nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa takwimu za hali ya hewa na kuboresha matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na uendeshaji wa shughuli za hali ya hewa hapa nchini.

MAJUKUMU YA TMA

Serikali kupitia Mamlaka hiyo imeendelea na utoaji wa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini. 

Majukumu mengine ni pamoja na kutoa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za hali mbaya ya hewa, kupima na kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutafiti kisayansi mabadiliko ya hali ya hewa nchini, kubadilishana taarifa za hali ya hewa katika mtandao wa mawasiliano wa dunia kulingana na makubaliano ya Kimataifa na kuiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.

Waziri Mbarawa ameeleza kuwa Serikali kupitia TMA imeendelea kutoa huduma za utabiri wa kila siku, siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ambapo usahihi wa utabiri umefikia asilimia 86 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). 

Ameeleza kuwa TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa kuanzia Januari 22 - 27 2024, na kuendelea kukidhi vigezo vya kumiliki cheti cha ubora (ISO 9001: 2015), katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Ibara ya 59(j) na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22-2025/26), Serikali iliahidi kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa rada.

"Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali kupitia TMA imekamilisha ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano  za hali ya hewa nchini," amesema Prof. Mbarawa.

Amefafanua kuwa utengenezaji wa rada nyingine mbili unaendelea kiwandani nchini Marekani na inatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu na kwamba rada hizo zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma nahivyo kukamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba za hali ya hewa nchini. 

Aidha amebainisha kuwa Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa.

Waziri huyo amesema katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga, Serikali ilikamilisha ufungaji wa mitambo mitano ya kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Songwe, Zanzibar, Mtwara, Arusha na Songea na kwamba taratibu za ufungaji wa mitambo mitatu ya kupima hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Musoma, Iringa na Mpanda zinaendelea.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU