Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
MKUU wa Sehemu ya Masoko na Uhamasishaji, kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB),David Maghali ameeleza kuwa kuna fursa kwa wawekezaji kuanzisha vituo vya kuchakata za la mkonge ili kuongeza thamani.
Hayo ameyasema leo Julai 5, 20225 katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba' amesema sekta ya mkonge inatoa fursa mbalimbali kwa Watanzania, ikiwemo kwenye uzalishaji wa Mbegu kutokana na mahitaji ya mbegu ni makubwa na ongezeko la wakulima wanaochangamkia zao hilo.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha mkonge, na kwamba ni muda muafaka kwa vijana na wawekezaji kujiunga katika sekta hiyo yenye faida nyingi ambazo changamoto zake ni chache ikilinganishwa na mazao mengine.
Maghali amesema kuwa lengo kuu la ushiriki wao katika maonesho hayo ni kuhakikisha kwamba wanawafikia wadau wa sekta ya mkonge pamoja na wananchi na kuwapatia elimu muhimu ili kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.
Ameongeza kuwa wanawaelimisha wakulima kuhakikisha wanazalisha mkonge unaokidhi viwango vya soko ndani na nje ya nchi na kwamba hilo ni zao lenye thamani kubwa na soko la uhakika.
Afisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Mkonge Emanuel Lutego,amesema kuwa Bodi hiyo inaendelea kuhimiza wananchi, hasa vijana na wawekezaji,kutumia fursa hii ya dhahabu kujiingiza katika kilimo, uchakataji na ubunifu wa bidhaa zitokanazo na mkonge.
Sekta ya mkonge nchini Tanzania ni chachu ya maendeleo ya viwanda na ubunifu wa bidhaa mbali na kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa wakulima.
0 Comments