Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MFUGAJI na mtaalam wa kilimo na mifugo kutoka jijini Dodoma, Christopher Dioniz, amesema kuwa anajihusisha na ufugaji wa kuku wa kienyeji, huku akitambulisha aina ya kuku wa kisasa wanaojulikana kama Ayam Cemani kutoka Indonesia.
Hayo ameyasema leo Agosti 5,2025 katika maonesho ya Wafugaji na wakulima Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini hapa amesema kuku hao wa Ayam Cemani, ambao kwa sasa wanapatikana jijini Dodoma, wanasifika kwa kuwa na thamani kubwa ya kitiba na lishe nchini Indonesia na China.
Dioniz amesema kuku hao si wa kawaida, kwani wanaaminika kusaidia afya ya binadamu kupitia virutubisho vilivyomo katika nyama yao.
“Kutokana na aina ya ufugaji ninaoufanya, natumia chakula cha kuku tulichotengeneza kwa ubora wa hali ya juu kinachoitwa Rehoboth Animal Feeds. Tupo hapa Dodoma, na ofisi zetu zipo maeneo ya Ipagala,” amesema Dioniz.
Ameeleza kuwa chakula hicho wanakitengenezwa kulingana na mahitaji ya aina mbalimbali za kuku, wakiwemo wa kienyeji, wa nyama, na chotara.
Pia amesema kuwa wanatoa huduma ya kufundisha namna ya kutengeneza chakula hicho kwa kutumia fomula maalum, sambamba na elimu ya ufugaji wa kuku kwa ujumla.
“Mbali na kutengeneza chakula cha kuku, tunauza pia vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya ufugaji. Katika maonesho haya tumeleta bidhaa mbalimbali za vyakula vya mifugo kwa ajili ya kuwahudumia wafugaji wanaohitaji ubora katika shughuli zao,” ameongeza Dioniz.
Dioniz ametoa wito kwa wafugaji kujiunga katika mfumo wa kisasa wa ufugaji unaozingatia lishe bora na mbinu sahihi za utunzaji wa kuku, ili kuongeza tija na kipato kupitia sekta hiyo ya mifugo.
0 Comments