Na Asha Mwakyonde,RUKWA
BENKI ya CRDB imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwaunga mkono vijana wenye mahitaji maalumu kwa kuwapatia fursa za kiuchumi zitakazowawezesha kujitegemea, kutumia ujuzi wao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Hatua hiyo imeonekana kupitia ziara ya viongozi wa benki hiyo katika banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),
kwenye Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mkoani Rukwa, ambapo ilinunua bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na vijana hao, zikiwamo nguo walizoshona wenyewe, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zao za kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza leo Oktoba 9,2026 katika maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta Maendeleo,”Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Sumbawanga, Ruhore Masaka, amesema benki hiyo inatambua umuhimu wa kuhakikisha vijana wote wanapata fursa za kiuchumi, wakiwamo wenye mahitaji maalumu.
Amesema vijana hao wana uwezo, vipaji na ari ya kujiletea maendeleo, hivyo ni muhimu kuwapatia mazingira na fursa zitakazowawezesha kutumia uwezo wao kujenga maisha bora.
"Sisi kama benki tunatamani vijana wote waweze kupata fursa sawa za kifedha kwa mfano vijana wenye mahitaji maalum tunawasapoti kwa kiasi kkiubwa mbali na taasisi sisi binafsi kama viongozi tumeguswa na vijana hawa, tumeona wanajituma, wanaujuzi kama benki tuna uwezo wa kuwasapoti kifedha ili waweze kujikimu mahitaji yao," amesema.
Masaka ameeleza kuwa benki hiyo imeguswa na juhudi zinazofanywa na vijana hao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuona umuhimu wa kuwaunga mkono ili waweze kutimiza malengo yao.
Amesisitiza kuwa CRDB itaendelea kuangalia namna bora ya kuwasaidia vijana hao kupata fursa za kiuchumi zitakazowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
“Dhamira ya benki hii ni kuhakikisha huduma na fursa zinazotolewa zinawafikia watu wote, hususan vijana wenye mahitaji maalumu, bila kuwaacha nyuma katika safari ya maendeleo,” ameeleza.
Ameongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya kuimarisha ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalumu katika shughuli za kiuchumi na kuwapa nafasi ya kutumia uwezo wao katika kujenga maisha bora.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano na Taasisi za Serikali wa Benki ya CRDB, Paskalina Diu, amesema benki hiyo ina programu na vitengo mbalimbali vinavyolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, ikiwamo kuwapatia mitaji wezeshi isiyokuwa na riba kupitia mifumo maalumu ya uwezeshaji.
Amesema kupitia CRDB Bank Foundation, benki hiyo itaangalia namna ya kuwasaidia vijana hao kupitia kliniki za ushauri na huduma mbalimbali zitakazosaidia kubaini mahitaji yao na fursa zinazoweza kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Diu ameeleza kuwa CRDB Bank Foundation inalenga kuwawezesha walengwa kupitia mitaji wezeshi isiyokuwa na riba na mipango mingine ya kuwasaidia kukuza shughuli zao za uzalishaji na kujitegemea kiuchumi.
Amebainisha kuwa miongoni mwa mipango hiyo ni programu ya Imbeju, iliyoanzishwa na CRDB Bank Foundation kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi nchini.
Naye Francis Madanganya, mbunifu wa kifaa cha kuchaji simu za mkononi (power bank), ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwaunga mkono vijana wenye mahitaji maalumu na kuwatambua kwa kazi wanazozifanya.
Madanganya amewahimiza vijana wenzake wenye ulemavu kutokata tamaa wala kujifungia nyumbani, badala yake wajitokeze kupata mafunzo katika vyuo vya ufundi stadi vya VETA ambako kuna fani mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kukuza ujuzi wao, kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.





0 Comments