TANZANIA, MSUMBIJI ZAKAZIA USHIRIKIANO WA ULINZI NA USALAMA


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

TANZANIA na Msumbiji zimeendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika ulinzi na usalama, huku zikisisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa pamoja kukabiliana na changamoto zinazotishia amani, utulivu na usalama wa nchi hizo na ukanda kwa ujumla.

Msisitizo huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Msumbiji (JPCC), uliofanyika leo Oktoba 5, 2026, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umefunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.

Faraji Mnyepe, katika Ukumbi wa The Aga Khan Diamond Jubilee, ukihudhuriwa na Makatibu Wakuu, wawakilishi wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wataalamu kutoka Tanzania na Msumbiji.

Akifungua mkutano huo, Dk. Mnyepe amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji katika diplomasia ya ulinzi na usalama una historia ndefu, iliyojengwa katika misingi ya ujirani mwema, urafiki na maslahi ya pamoja ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Ameeleza kuwa mkutano huo ni fursa muhimu kwa pande zote mbili kutathmini kwa pamoja masuala ya ulinzi na usalama, kubadilishana uzoefu na utaalamu, pamoja na kujadili maeneo mapya ya kuimarisha ushirikiano.

Dk. Mnyepe amewataka wajumbe na wataalamu kutumia fursa hiyo kujadili kwa kina masuala yaliyo kwenye ajenda ya mkutano kwa mtazamo wa pamoja, ili kufikia maazimio yenye tija na yanayoweza kutekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya Tanzania na Msumbiji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji, Casimiro Augusto Mueio, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri na ukarimu ulioonyeshwa kwa ujumbe wa Msumbiji tangu ulipowasili nchini.

Mueio ameeleza matumaini kuwa majadiliano katika mkutano huo yatawezesha nchi hizo kupata suluhisho la pamoja kuhusu masuala mbalimbali ya ulinzi na usalama, hatua itakayosaidia kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Msumbiji.

Amebainisha kuwa ushirikiano huo una umuhimu mkubwa kwa nchi hizo mbili na wananchi wake, hasa katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazohitaji mshikamano na hatua za pamoja.

Tanzania na Msumbiji zina historia ndefu ya uhusiano wa kidiplomasia uliojengwa kwa kiasi kikubwa wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ambapo Tanzania ilitoa mchango muhimu katika kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Msumbiji na mataifa mengine ya ukanda huo.

Msingi huo wa kihistoria umeendelea kuwa nguzo katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi hizo katika maeneo mbalimbali, hususan ulinzi na usalama, kwa lengo la kulinda amani, utulivu na maslahi ya pamoja.

Mkutano huo wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama unalenga, pamoja na mambo mengine, kupitia utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa na pande hizo mbili, kubaini maeneo mapya ya ushirikiano na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama zinazozikabili nchi hizo na ukanda kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments

TARURA NJOMBE YAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA