BRELA YAWAKARIBISHA WANANCHI KUTEMBELEA MABANDA YAO

Baadhi ya  watu waliotembelea moja ya mabanda ya wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wakipatiwa huduma.

NA ASHA MWAKYONDE,MBEYA

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imesema imeshahudumia watu zaidi ya 195 hadi kufikia tarehe 6 Agosti, 2022 waliotembelea banda hilo na kupata huduma za kurasimisha biashara zao, katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji maarufu Nanenane, yanayofanyika kitaifa jijini hapa.

Akizungumza katika moja ya mabanda ya BRELA, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kutoka Taasisi hiyo, Roida Andusamile amesema hadi kufikia mwisho wa maonesho hayo  wanaamini idadi itaongezeka na watakuwa wamewafikia wadau wengi  kwa kutoa huduma za papo kwa papo.

Mkuu huyo wa Kitengo ameongeza kuwa gharama za usajili ni nafuu kabisa ambapo kusajili jina la biashara ni TZS 20,000  na kuhusu kampuni inategemea na mtaji wa mfanyabiashara.

"BRELA tunashiriki katika maonesho haya ya wakulima na wafugaji ambapo  kaulimbiu ya mwaka huu ni "Agenda 10/30, Kilimo  ni Biashara Shiriki Kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi," na sisi ni wadau wa biashara tunarasimisha na kuwezesha  biashara  kwa wadau mbalimbali wanaojihusisha na biashara," amesema Andusamile.

Andusamile amesema huduma wanazozitoa ni usajili wa majina ya biashara, kampuni, alama za biashara na huduma, utoaji wa hataza, leseni za biashara kundi 'A', leseni za viwanda pamoja na usajili wa viwanda vidogo.

Mkuu huyo wa Kitengo amesema kuwa BRELA wanatoa leseni za biashara kundi A, ambazo zina mtazamo wa Kitaifa na kimataifa huku akifafanua kuwa kuna leseni zinazotolewa na Halmashauri ambazo ni kundi B.

Andusamile amesema  BRELA ni wadau wakubwa katika monesho hayo kutokana na majukumu ambayo inayafanya kuhakikisha mkulima anafanya biashara kulingana na mazao anayozalisha.

"Tuna  wanawahamasisha wananchi wa Mbeya kutumia fursa ya maonesho hayo  kutembelea mabanda ya BRELA ili kupata elimu na ushauri kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara zao," ameeleza.

Post a Comment

0 Comments

KONGAMANO LA ARGeo-C10 LINALENGA KUONGEZA KASI YA UENDELEZAJI JOTOARDHI AFRIKA- DKT. MATARAGIO