SERA YA JINSIA NA MAENDELEO YA WANAWAKE MBIONI


 Na WMJJWM, DSM, 15 Agosti, 2022.

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amepokea Rasimu ya Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ambayo imefikia hatua nzuri baada ya kufanyiwa maboresho na kuwafikia wadau wengi zaidi.

Waziri Dkt. Gwajima akipokea wasilisho la Sera hiyo Agosti 15, 2022 amesema, anauona mwangaza baada ya Kikosi kazi hicho kwenda kuchukua maoni zaidi kwa wadau.

"Prof. Linda Mhando pamoja na jopo lako niwapongeze kwa hatua hii, kwakweli mmejaribu kuja na wasilisho ambalo linajibu mahitaji ya dunia ya sasa katika kuchochea maendeleo ya Jinsia na Wanawake hivyo, hatua inayofuata ni kuwashirikisha zaidi wadau mbalimbali ili tuone wapi paboreshwe" amesema Waziri Dkt. Gwajima 

Akiwasilisha Rasimu hiyo, Mshauri Elekezi Prof. Linda Mhando alisema kuwa, walizingatia maelekezo ya awali waliyoyapokea kutoka kwa Waziri ikiwepo kulifikia kundi la Vijana sambamba na wadau wa Asasi za Kiraia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Zainab Chaula akimkaribisha Waziri kupokea Rasimu hiyo alimuelezea Waziri kuwa Kikosi kazi hicho kimezingatia maelekezo ya Waziri ikiwepo kupokea maelekezo ya wadau ambao hapo awali hawakujumuishwa. 

"Mhe. Waziri nikipongeze Kikosi hiki ambacho ulielekeza nikiunde, lakini baada ya kupokea Rasimu ya kwanza ulihitaji yafanyike maboresho, niseme maboresho yamezingatia maoni tuliowapa awali" Dkt. Chaula. 

Nao baadhi ya Wakurugenzi na wataalam wa Wizara, walioshiriki kwenye hafla hiyo ya kupokea sehemu rasimu ya Sera hiyo wamekishukuru Kikosi kazi kwa kazi waliyokabidhiwa na wanaimani Sera hiyo kukamilika kwake itakuwa na manufaa kwa Jamii ya Watanzania.

Mapema Mwezi Julai, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula aliteuwa Kikosi kazi cha watu kumi kwaajili ya kuandaa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya 2022, kutokana na iliyokuwa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000.


Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA