TAEC YATOA ELIMU MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA MAJI



NA ASHA MWAKYONDE,MBEYA 

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), imeendelea kutoa elimu namna ambavyo teknolojia ya Nyuklia inavyoboresha Sekta za kilimo, mifugo na rasilimali za maji hapa mchini.

Shirika la Chakula Duniani (FAO) na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) ambapo Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ni wanachama wamekuwa wakipanua maarifa na kuongeza uwezo katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50 na matokeo na mafanikio makubwa yanaonekana ulimwenguni kote kupitia teknolojia hiyo.

Akizungumza jijini Mbeya katika maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu Nane yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale ambapo kitaifa yanafanyika mkoani hapa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAEC,Peter Ngamilo ameelezea kwa kina juu ya teknolojia hiyo ya nyuklia inavyoboresha sekta hizo.

Ngamilo amesema teknolojia ya Nyuklia hutumika kuboresha mazao ya Kilimo, Mifugo sanjari na utafutaji na uboreshaji wa rasilimali ya maji.

Amesema matumizi ya Teknolojia ya Nyuklia duninai ni makubwa na teknolojia hiyo imekuwa mkombozi katika kutokomeza wadudu waharibifu katika mazao yatokanayo na kilimo na mifugo, hivyo kupunguza kuenea kwa wadudu na magonjwa, kuongeza uzalishaji wa mazao, kulinda rasilimali za ardhi na maji, kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza uzalishaji wa mifugo.

Ngamilo ameainisha mifano mbalimbali ya jinsi ambavyo Teknolojia ya Nyuklia inavyoboresha kilimo na mifugo katika nchi wanachama wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kama ,Uzalishaji wa wanyama na uboreshaji wa afya za mifugo,Uboreshaji wa udongo na maji, Usimamizi wa Wadudu, Usalama wa chakula.

Nyingine ni Mabadiliko ya hali ya hewa, Kuzuia njaa ya msimu, na Ukabilianaji na Janga inapotokea dharura (Alama ya Taadhari ya Uwepo wa Mionzi)

"Katika uzalishaji wa wanyama na uboreshaji wa afya za mifugo Teknolojia ya Nyuklia hutumika na kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta za kilimo na mifugo katika kuongeza uzalishaji wa mifugo, kudhibiti na kuzuia magonjwa mtambuka ya wanyama na kulinda mazingira," amesema Ngamilo.

Ngamilo ametolea mfano jinsi ya teknolojia ya nyuklia ilivyotumika Zanzibar na kuweza kupata mbegu bora ya mpunga aina ya Supa BC, ambapo amesema kuwa awali wakulima wa Zanzibar kabla ya utafiti na ujio wa mbegu hiyo.

Ameongeza kuwa kwa wastani katika hekta moja mkulima alikuwa anapata gunia za mpunga chini ya kumi, lakini baada ya utafiti uliotoa matokeo ya mbegu ya mpunga ya SUPA BC, katika hekari moja mkulima ameweza kupata wastani wa tani 7 na kuendelea. 

"Mbegu ya SUPA BC inavumilia ukame, haipati magonjwa kirahisi, haishambuliwi na wadudu na mchele wake una ladha na kutoa harufu nzuri. 

“Vilevile teknolojia ya nyuklia imetumika kumaliza Mbung’o ambao walikuwa wakitishia maisha ya mifugo huko Zanzibar ambapo mpaka sasa mafanikio yake ni makubwa na kufanya tatizo la Mbung’o kuwa historia tofauti na ilivyokuwa hapo awali,"amesema Ngamilo.

Akiendelea kufafanua Ngamilo ametoa mfano wa nchi ya Cameroon kuwa imetumia vyema Teknolojia ya Nyuklia katika uzalishaji wa mifugo na kutokomeza wadudu waharibifu, hivyo kudhibiti magonjwa na kupelekea wakulima kuongeza mazao yao ya maziwa mara tatu kutoka lita 500 hadi 1500 na kutoa nyongeza ya dola Milioni 110 katika mapato ya mkulima kwa mwaka. 


Post a Comment

0 Comments

BARABARA YA LAMI YA KM 7.7 YENYE THAMANI YA BILIONI 9.3 KUUNGANISHA MIKOA YA SINGIDA-SIMIYU-ARUSHA