VETA: MKULIMA BILA UJUZI HAWEZI KUENDESHA KILIMO


NA ASHA MWAKYONDE, MBEYA

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imesema kuwa mkulima hawezi kuendesha kilimo cha biashara bila kuwa na ujuzi hivyo inawahamasisha kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ambayo hutolewa kwenye maeneo mbalimbali yakihusisha ufundi wa zana za kilimo na Ufugaji wa mifugo.

Akizungimza jijini Mbeya Agosti 4,2022 katika maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu nane nane yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale ambapo kitaifa yanafanyika mkoani hapa,Meneja Uhusiano VETA, Sitta Peter amesema mkulima bila kuwa na ujuzi hawezi kuendesha kilimo cha biashara ambacho kitamletea tija

Amesema kuwa wanashiriki katika maonesho hayo wakienda sanjari na agenda ya 10/30 yenye kaulimbiu inayosema "Kilimo ni Biashara Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo Ufugaji na Uvuv" kupitia kaulimbiu hiyo Veta imejipanga kuzungumzia mambo makuu mawili.

Meneja huyo wa Uhusiano amesema jambo la kwanza ni kuelimisha watu juu ya fursa zinazopatikana VETA kwani mkulima hawezi kuendesha kilimo cha biashara bila kuwa na ujuzi wa zana za kilimo.Amesema jambo la pili VETA inahamasisha suala la Sensa ya Watu na Makazi ambayo inatarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu wananchi washiriki kuhesabiwa ili kuisaidia serikali kupanga mipango ya maendeleo.

Meneja huyo amefafanua kuwa wananchi wakishiriki kuhesabiwa wataisaidia serikali kujua mahitaji ya ujuzi huku akibainisha kuna vijana wengi ambapo kwa sasa hawawatambui wanao waona wakienda kuhitaji mafunzo.

Amesema wananchi wakishiriki kuhesabiwa watawatambua vijana wapo kiasi gani ili kuweza kuandaa miundombinu ya mafunzo itakayowatosheleza mahitaji yao.

"VETA tunashiriki kwenye maonesho haya ya nane nane kitaifa hapa mkoani Mbeya, tunatumia fursa hii kuwaelimisha wananchi juu ya fursa za elimu ya ufundi na mafunzo stadi hususan mafunzo yanayolenga sekta ya kilimo na mazao mbalimbal, ufugaji pamoja na teknolojia" amesema.

Ameongeza kuwa mamlaka hiyo ina teknolojia mbalimbali zinazogusa uchakataji wa mazao ya kilimo, urutubishaji wa udongo, umwagiliaji na nyingine ambazo wakulima wakizitumia zitaongeza tija kwenye sekta ya kilimo na kusaidia kuwa wa kidigitali.

Post a Comment

0 Comments

TANZANIA KUJIFUNZA TEKNOLOJIA YA MAGARI YA UMEME SINGAPORE - DKT. BITEKO