WATOTO ZAIDI 400,000 HAWAJAPATA CHANJO KWA KIPINDI CHA MIAKA MITATU


NA ASHA MWAKYONDE, DODOMA

WAZIRI  wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara imebaini zaidi ya watoto 400,000 wenye umri  chini ya miaka 5 hawajapata chanjo kabisa na kwamba lipo kundi jingine la watoto hao hawajakamilisha katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hayo ameyasema leo jijini hapa wakati akitoa taarifa kwa Umma kuhusu ongezeko la wagonjwa wa surua nchini  amesema baada ya ongezeko hilo  Wizara imefanya tathmini ya mwenendo wa utoaji wa chanjo za watoto ili kubaini idadi ya watoto hao  wanaopata na kukamilisha  kwa kuzingatia ratiba.

Amesema  tathmini iliyofanyika  kwa kuchambua takwimu za miaka mitatu  mfulilizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 imeonesha kiwango cha  utoaji wa chanjo watoto hao nchini kimeshuka  na kinaendelea kushuka.

"Mikoa yenye watoto wengi ambao hawajapata chanjo (Ziro dose),ni Kigoma,Kagera, Mara, Songwe,Manyara na Mbeya huku akisema kuwa mikoa yenye watoto ambao hawajakamilisha ni Tabora, Dar es Salaam, Arusha, Geita,Rukwa, Shinyanga,  Pwani, Singida,Ruvuma, Dodoma, Manyara, Kigoma,Morogoro,Lindi, Songwe, Mtwara, Katavi, Iringa na Mbeya," amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameeleza kuwa moja ya sababu zinazotajwa kuathiri utoaji wa chanjo ni janga la UVIKO- 19 na kwamba sababu hiyo haijaathri Tanzania tu nchi nyingine duniani.

Amefafanua kuwa hali hiyo ya uwepo wa idadi kubwa ya watoto ambao hawajapata  chanjo  au kukamilisha ikiwamo ya surua inaiweka nchi katika hatari ya kupata milipuko ya magonjwa hususani yale yanayozuilika.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa chanjo wa Taifa Dk. Florian Tinuga amesema  chanjo za watoto zipo za aina tisa kati ya hizo saba ni wa watoto waliochini ya miaka mitano, moja ni ya wasichana wenye miaka 14 ambayo inazuia saratani ya shingo ya kizazi na moja ni ya tetenasi  ambayo wanaopata wanawake wajawazito na walio katika umri wa kubeba mimba.

Amefafanua kuwa katika chanjo hizo kuna ambazo zinazuia magonjwa yanayozuilika ambayo ni polio,akili na surua na tetenasi.

" Kwa miaka mingi nchi yetu imekuwa ikifanya vizuri kwenye haya magonjwa kwa ugonjwa wa polio mgonjwa wa mwisho alikuwa mwaka 1996 hivyo tuna muda mrefu hatuna mgonjwa wa polio lakini kuna kipindi tunapata wagonjwa wa surua na ugonjwa wa tetenasi kwa watoto hatuna muda mrefu," amesema.

Ameongeza wamefanikiwa  kudhubiti magonjwa hayo kwa kuwa wana mfumo wanaotumia wa hali ya ufuatilia kwa ukaribu wa magonjwa  hayo ambao upo katika ngazi ya Taifa hadi vituo.


Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI