WAZIRI UMMY: KUNA HATARI YA BIMA YA NHIF KULEMEWA NA GHARAMA


 NA ASHA MWAKYONDE,DODOMA 

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa kuna hatari ya Mifuko wa Taifa wa   Bima ya Afya (NHIF), kulemewa kutokana na  ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuwa na mzigo mkubwa endapo hatua stahiki hazitachukuliwa katika kudhibiti magonjwa hayo.

Pia amesema takwimu zilizopo,gharama za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 35.65 mwaka 2016 na 2017 hadi shilingi bilioni 99.09 mwaka 2021/22.

Akizungimza jijini hapa leo Septemba 1, 2022 na waandishi wa habari wakati akitoa hali ya mfuko wa NHIF, Waziri Ummy amesema kuna hatari ya mfuko huo kulemewa na gharama za matibabu.

Waziri huyo ameeleza kuwa kuna idadi kubwa  ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa hivyo katika kuimarisha huduma za afya serikali inafanya juhudi kubwa ya kuhakikisha inatokomeza magonjwa hayo lakini bado kuna changamoto ya kuongezeka kwa idadi hiyo.

Amesema kuwa gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi na chemotherapia (chemotherapy services), kupitia Mfuko ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 22.5 mwaka 2021/22.

Waziri Ummy amefafanua kuwa matibabu ya figo kwa wanachama wanaopata huduma ya kuchuja damu (hemodialysis services), gharama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9.5 mwaka 2015/16 kufikia shilingi bilioni 35.44 mwaka 2021/22. 

"Idadi ya wagonjwa hawa wa figo imeongezeka kutoka 280 mwaka 2014/15 hadi kufikia 2,099 mwaka 2021/22.Gharama za matibabu ya moyo kwa wanachama wa Mfuko wanaopata matibabu ya upasuaji wa moyo (minimal and invasive cardiac procedures), ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 4.33 mwaka 2021/22," ameeleza.

Aidha Waziri huyo amebainisha kuwa gharama za vipimo vya CT scan na MRI ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 5.43 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10.87 mwaka 2021/22.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy takwimu hizi, ni wazi kuwa kama hatutachukua hatua madhubuti kama nchi, kuna uwezekano wa Mfuko kwa siku za mbeleni kushindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Aidha Waziri Ummy ameelekeza NHIF kuimarisha mikakati yake ya kupambana na vitendo vya udanganyifu pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.

"Changamoto nyingine iliyopo ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni wagonjwa," amesema Waziri Ummy.

Ameongeza kuwa Makundi haya ni kutoka katika Sekta rasmi binafsi pamoja na ile isiyo rasmi ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2022, Mfuko unahudumia takribani wanufaika milioni 4.8 ikilinganishwa na wanufaika 691,173 waliokuwa wakihudumiwa mwaka 2001/02.  

"Uwepo wa takribani asilimia 99 ya wanachama waliojiunga kwa hiari ambao ni wagonjwa imekuwa ikiongeza gharama za matibabu zinazolipwa na Mfuko," amesema.

Aidha amewatoa wasiwasi wadau wa NHIF wakiwemo wanachama, watoa huduma pamoja na watanzania wote kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa Mfuko huu unakuwa imara, endelevu na stahimilivu kwani kwa sasa, ni moja kati ya mfumo unaotumika katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa nchini.

Pamoja na kuwa na wanachama asilimia nane (8)  ya Watanzania wote, vituo vingi vya kutolea huduma vinategemea mapato kutoka katika Mfuko kwa zaidi ya asilimia 70.




Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Benard Konga amesema kuwa wanaofanya ubadhilifu wa fedha wanawapeleka katika Taasisi  ambazo zinahusika na uchunguzi na wakibainika lazima hatua zichukuliwe dhidi yao.

" Wamiliki tunawapeleka kwenye Taasisi za kiserikali ambazo zinahusika na uchaguzi lakini pia tumebaini  baadhi ya wanachama ambao sio waaminifu wana wapatia ndugu zao kadi tumezuia zile huduma ambazo anazipata," amesema Mkurugenzi huyo.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA