MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA YAPUNGUA NCHINI KWA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA


 Na Asha Mwakyonde, Dodoma

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Gerald Kusaya,amesema kuwa biashara na matumizi ya dawa za kulevya yamepungua katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Disemba 2021 hadi Disemba 2022

Akizungumza Jijini Dodoma leo Januari 25,2023, katika banda la Mamlaka hiyo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square, amesema biashara na matumizi ya dawa hizo hapa nchini yamepungua kutokana na Watanzania wengi waliokuwa wanajihusisha na dawa za kulevya wengi wao wameamua kuacha na matumizi hayo.

Kamishna Jenerali huyo ameeleza kuwa mapambano yanaongezeka kwa maana wale wahalifu,wauzaji na watumia wameingia uraiani na wao kama serikali wanahakisha wapo nyuma yao.

Ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja Mamlaka hiyo kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameweze kukamata jumla ya kilo 11990 za dawa za kulevya za aina mbalimbali.

Amefafanua kuwa katika dawa hizo ambayo imeongoza ni bangi kilo 6900 na ya pili ni mirungi kilo 4500, zinazofuatia ni Heroin, Cocaine na nyingine ni kiasi kidogo.

"Hadi sasa kwa takwimu za leo tuna watu12,800 ambao wamejisalimisha kwa serikali na wanataka kupatiwa matibabu, serikali inaendelea kuwapatia matibabu ya kila siku. Hii ni takwimu kubwa sana ikilinganishwa na miaka mitano ya nyuma iliyopita," amesema Kamishna Jenerali huyo wa DCEA.

Kamishna Jenerali Kusaya amefafanua kuwa yapo matumizi ya dawa tiba nyingine za binadamu zenye asili ya kulevya kama Valium, Tramadol na Pethidine zimekuwa zikitumika kama dawa za kulevya na kwamba mapambano yanaendelea hayaishii hapo.

Amesema wamekuwa wakipambana katika suala zima la kuhakikisha wanapambana na wale ambao wanaingiza kemikali Bashirifu kwa matumizi ambavyo hayaruhusiwi .

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali huyo katika kipindi kilichopita wameweza kuzuia uingizaji wa takribani kilo 120,000 za dawa za kemikali Bashirifu na kuzuia lita 85 za kemikali hizo kwa kuwa zikiingia nchini bila Kudhibitiwa watu wanaweza kutumia kutengeneza dawa za kulevya nyumbani na mitaani.

"Sisi ni Mamlaka ni wadau wa moja kwa moja ndio maana tumeweza kushiriki katika maonesho haya, sisi ni taasisi ya Umma ambayo ipo Kisheria tunafanya kazi zetu kimsingi na tumesajiliwa kwa sheria Namba 5 ya mwaka 2015," amesema.

Ameeleza kuwa lengo la kushiriki maonesho hayo ni kutaka kuelemisha Watanzania kuhusiana na sheria ambayo imeunda Mamlaka hiyo na kusema ni vizuri wananchi wakapata fursa kuifahamu sheria inasemaje kuhusiana na makosa mbalimbali inayohusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya na inaeleza ni adhabu gani anaweza kupata akikutwa na kiasi gani na ni aina gani za dawa hizo.

Kamishna Jenerali amefafanua kuwa maonesho hayo kwao ni sehemu nzuri ya kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa ni mambo ambayo yapo wazi ni vizuri wananchi wakafahamu sheria inayounda mamlaka hiyo na madhara mbalimbali yanayotokana na dawa hizo.

"Sio madhara tu je nani anaweza akapata nini, mtu atakapokutwa akijihusisha na biashara hii, tunaangalia katika nyanja zote lakini tunaamini wazi kila mtanzania aweze kufahamu madhara yanayotokana na dawa za kulevya, kikubwa ni kumuelimisha hii ni njia mojawapo ya kuhakikisha kila mtanzania atakayefika katika viwanja hivi madhara ya dawa hizi," amesema.

Amesema kuwa Watanzania wengi wakifahamu madhara ya dawa za kulevya ndipo wataichukia biashara ya dawa hizo na matumizi yake ndipo wataingia katika mapambano na kupata Tanzania isiyo na dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali huyo amesema hilo linawezekana kwa kuwa biashara na matumizi ya dawa hizo yanaiharibu jamii na kwamba hakutakuwa na nguvu kazi kama vijana na Watu wazima wakiendelea kutumika dawa za kulevya.

Amewataka Watanzania wajiepushe na dawa za kulevya kwa kuwa madhara yake ni makubwa pamoja na adhabu zinazotokana matumizi hayo na pengine kumuharibia mpangilio wake maisha.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI