NAIBU WAZIRI WA MAJI AMPONGEZA MKURUGENZI MTENDAJI WA SUWASA


 Singida 

NAIBU Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb) amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Sebastian Warioba kwa kazi nzuri ya utendaji wa Mamlaka ambapo katika usimamizi wake SUWASA imeongeza makusanyo kutoka wastani wa shilingi milioni 290 kwa mwezi mwezi Mei 2022 hadi shilingi milioni 380 kwa mwezi kufikia mwezi Oktoba 2024.

Aidha Mhe. Kundo ametoa pongezi pia kwa jitihada kubwa za kudhibiti upotevu wa maji ambapo mwezi Mei 2022 upotevu wa maji ulikuwa wastani wa asilimia 33.3 na kwa sasa umeshuka na kuwa wastani wa asilimia 25. Vilevile ametoa pongezi kwa kuongeza wateja wapya kutoka 15,119 Mwezi Mei 2022 hadi wateja 21,211 mwezi Novemba 2024. 

Mhe. Naibu Waziri ametoa pongezi hizo akiwa katika Ziara ya Kikazi Mkoa wa Singida ambapo amefanya kikao na Menejimenti za Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji Mkoa wa Singida ambazo ni Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), RUWASA, Bonde la Kati, Maabara ya Ubora wa Maji, Chuo cha Maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kiomboi (KIUWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manyoni (MAUWASA).

Katika kikao hicho kilichofanyika Ukumbi wa Bonde la Kati, Mhe. Kundo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA kwa usimamizi mzuri wa Taasisi ambao umeiwezesha SUWASA kupiga hatua, baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya Maji ya SUWASA.

Akieleza mafanikio ya SUWASA kuanzia mwaka 2022 mpaka 2024 Mkurugenzi Mtendaji Sebastian Warioba amesema mwaka 2023/2024 SUWASA imefanikiwa kupokea fedha kiasi cha shilingi Bil 1.3 kutoka serikali kuu zilizowezesha Ununuzi wa Dira 20,106 za malipo baada fedha kutoka Serikali kuu ambapo kutekeleza Miradi mbalimbali ya Maji kama Mradi wa Unyambwa na Ulemo Misigiri.

Aidha kupitia Mapato ya ndani, SUWASA imetekeleza miradi ya Uboreshaji wa huduma ikiwemo mradi wa Manga wa milioni 92.2 ikishirikiana na Shirika la Direct Aid Society, Ufufuaji wa Visima 12 vya Mkono maeneo ya Unyakumi, Unyianga na Mtamaa kwa gharama ya shilingi milioni 17.2, Kuongeza Mtandao wa Majisafi kwa kilometa 11.1 kwa gharama ya shilingi milioni 487.8 katika maeneo ya Manguamitogho, Mungumaji, Minga na Mandewa. Aidha SUWASA imejenga kituo kimoja cha kuchotea Maji shule ya msingi Kisiluda Irisya, na kujenga mfumo wa kutibu maji Kisima cha TCRS ambapo uboreshaji huu una thamani ya shilingi milioni 120.1

Kutokana na maboresho hayo SUWASA imefanikiwa kuongeza Mapato yake ya ndani kutoka shilingi milioni 290 mpaka milioni 380 kwa mwezi na kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 33.3 kufikia asilimia 25.

Mhe. Kundo amezitaka Menejimenti za Taasisi zote kufanya kazi kwa bidii, kuongeza ubunifu katika utendaji na kuimarisha ushirikiano na Upendo ili kuendelea kuboresha hali ya huduma kwa wananchi.

Mhe. Naibu Waziri anaendelea na ziara yake tarehe 3 Desemba kwa kutembelea Mradi wa uchimbaji visima 900 Nchini ambapo Singida Ina visima 40, Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Majitaka Manga Manispaa ya Singida na Mradi wa Miji 28 Manyoni.







Post a Comment

0 Comments

MABADILIKO YALETA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA SEKTA YA AFYA TANZANIA