Moja ya madarasa ya elimu ya awali yaliyoboreshwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni mwaka huu.
📍Fahamu ilivyotatua changamoto zake na ufuatiliaji wa miradiNa Asha Mwakyonde DODOMA
UTENDAJI kazi wa Halmashauri ya Mji Kondoa kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Juni mwaka huu imejielekeza namna ilivyotoa huduma kwa wananchi za kijamii, kiuchumi na kisiasa na kielimu ikiongozwa na dhamira ya Halmashauri hiyo ya kutoa huduma bora za kwa wananchi na wakati.
Hivi karibuni Halmashauri hiyo imetoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika idara zake ikiwamo Idara ya Elimu ya Awali na Msingi katika kipindi hicho.
Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Kondoa Said Majaliwa anazungumzia utekelezaji,uratibu, uhamasishaji, ufuatiliaji miradi, uandikishaji wa wanafunzi, changamoto na utatuzi katika idara hiyo kupitia taarifa ya baraza la madiwani la mwisho wa mwaka 2023/2024.
Akizungumzia utekelezaji Idara imefanya ufuatiliaji wa Taaluma Shuleni kuanzia mwezi Julai, 2023 hadi Juni, 2024 na kwamba ufuatiliaji huo ulilenga kukagua hali ya taaluma na kutoa maelekezo ya maboresho ya utendaji kazi jumla ya Shule 38 zilitembelewa.
Mkurugenzi huyo anazitaja shule hizo kuwa Mtakatifu Gema, Serengenyi, King’ang’a, Bolisa, Itiso, St Peter, Bicha Islamic, Kondoa, Kichangani, Tungufu, Mpalangwi, Migungani, Kwamtwara, Iyoli, Tampori, Kilimani na Kolowasi.
Anafafanua kuwa Shule zingine ni Hachwi, Choka, Ubembeni, Kondoa Shalom, Kingale, Kondoa Intergrity, Kondoa Islamic, Ibra, Munguri, Chandimo, Mongoroma, Tumbelo, Unkuku, Iboni, Miningani, Gubali, Maji ya Shamba, Chemchem, Lady Zahaar na vituo shikizi vinne vya Damai Kingale chini, Msui na Kotumo.
Majaliwa anaongeza kuwa ufuatiliaji wa Taaluma na shughuli mbalimbali zinazohusiana na ufundishaji na ujifunzaji huripotiwa Mkoani na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),kila siku ya Alhamisi na kupitia viashiria muhimu vya utendaji, 'key performance indicators' (KPI).
KURATIBU
Anaeleza kuwa wameratibu uendeshaji wa Mitihani ya pamoja ya Halmashauri hiyo ya kila mwezi kwa wanafunzi wa darasa la Saba na la nne pamoja na Usahihishaji wa Mitihani ya Mock Wilaya na Mock Mkoa wa Dodoma.
"Idara inaandaa Mitihani kwa darasa la Saba na la nne ambapo hufanyika katika kila shule zenye Madarasa ya Mtihani na katika Kipindi cha Julai 2023 hadi Juni mwaka huu tumekuwa tukifuatilia utolewaji wa Mitihani ya Kujipima inayoandaliwa na Afisa Elimu Kata, Mitihani ya Mock Wilaya na Mock Mkoa ambapo ufaulu wa Mitihani ya kimkoa ni 85 na Wilaya tumeweka lengo la 90," anasema.
Anaongeza kuwa katika kipindi cha Mwaka 2023/2024 Idara iliendelea kuratibu zoezi la usahihishaji Mitihani ya Mock Wilaya na Mock Mkoa kwa shule 35 hadi 38 ikiwa washiriki ni Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu na Walimu wa Taaluma kwa kubadilishana shule za kusahihisha lengo likiwa ni qkukutana kwa pamoja na kukamilisha zoezi hilo na Matokeo Kutumwa Mkoani.
UHAMASISHAJI
Anasema Halmashauri ya Mji Kondoa kupitia idara hiyo imefanya uhamasishaji wa utoaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi ambapo walikaa vikao na Wazazi, Walezi ili kuongeza ufanisi katika kujifunza.
"Idara imefanya ufuatiliaji na kuhamasisha utoaji lishe shuleni katika Shule za Msingi 28 kati ya 30 za Serikali na 7 kati ya 8 shule binafsi nazo zimefanikiwa kutoa chakula cha mchana kuanzia madarasa ya Awali hadi darasa la Saba.
Akizitaja baadhi ya shule hizo kwa ni Munguri, Mongoroma, Itiso, Bolisa,Ukunku, Ubembeni, Miningani, Kichangani,Maji ya Shamba, Mpalangwi, Kilimani, Bicha, King’ang’a na Kondoa kupitia michango ya Wazazi na Elimu ya Kujitegemea.
"Hadi Juni 30, mwaka huu jumla ya Wanafunzi 10897 wanapata chakula kati ya wanafunzi 16951 wa Shule za Serikali sawa na asilimia 64.2," anaeleza Mkurugenzi huyo.
MITIHANI YA TAIFA
Anasema Idara ilisimamia ufanyikaji wa Mitihani ya Taifa ya darasa la saba (PSLE), mwezi Septemba, 2023 na darasa la nne (SFNA) mwezi Oktoba mwaka huo," anaeleza Mkurugenzi huyo.
Nyumba ya walimu Shule ya Msingi Hachwi katika kuboresha mazingira ya walimu kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni mwaka huu.
UFUATILIAJI MIRADI
Mkurugenzi huyo anasema ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa na vyoo kwenye shule mbalimbali za Serikali katika kipindi cha Mwaka 2023/2024 Idara ilisimamia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Elimu Maalum Shule ya Msingi Iboni na Ukaraba wa madarasa matatu na ujenzi wa madarasa sita wa Shule ya Msingi Kondoa, na ujenzi wa Matundu nane ya vyoo katika Shule ya Msingi Kingale na Serengenyi.
Anaongeza kuwa miradi yote ilipokea fedha kutoka Serikali Kuu na Taasisi ya Elimu Tanzania, hadi kufikia Juni 30, mwak huu miradi yote hiyo ilikuwa imekamilika.
UANDIKISHAJI
Majaliwa anasema uandikiashaji hadi kufikia Juni mwaka huu jumla ya wanafunzi wa Awali walioandikishwa ni 2251 wakiwemo Wavulana 1158 na Wasichana 1093 na kwa darasa la kwanza walioandikishwa ni 2773 wakiwemo Wasichana 1333 na wavulana 1440.
UFANYIKAJI WA VIKAO
Anasema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi 1, Juni 3 mwaka huu Idara imekuwa ikifanya vikao na walimu wakuu wote kwa lengo la kuwapatia mwelekeo wa nini kifanyike katika kusimamia ufundishaji na maendeleo ya taaluma kwa ujumla.
"Mei 30 mwaka huu Idara iliratibu ufanyikaji wa kikao cha Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Elimu na Walimu wote wa Halmashauri ya Mji Kondoa, masuala mbalimbali yalitolewa ufafanuzi hasa suala la Upandaji Madaraja, Malimbikizo ya Mishahara, Likizo, Uhamisho, Matibabu na Masuala mbalimbali ya kinidhamu," anaeleza.
CHANGAMOTO
Akizungumzia changamoto za ufuatiliaji taaluma shuleni anasema kuwa hakuna changamoto zilizojitokeza za kukwanisha zoezi la ufuatiliaji shuleni.
Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa katika kuratibu uendeshaji wa Mitihani ya pamoja ya Halmashauri ya kila mwezi kwa wanafunzi wa darasa la saba na nne usahihishaji wa Mitihani ya Mock Wilaya na Mock Mkoa wa Dodoma hapakuwa na changamoto zilizojitokeza mitihani yote hufanyika kama ilivyo pangwa.
Akizungumzia uhamasishaji wa utoaji wa chakula shuleni anasema upatikanaji ni hafifu wa chakula cha mchana.
"Ufanyikaji wa Mitihani ya Taifa hakuna changamoto iliyojitokeza na ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule mbalimbali za Serikali na katika uandikishaji pia hakuna changamoto zilizojitokeza," anaeleza Majaliwa.
UTATUZI WA CHANGAMOTO
Anasema zoezi la ufuatiliaji taaluma shuleni ni endelevu na kwamba wanaendelea kuratibu na kuendesha mitihani ya kila mwezi huku akisema mitihani hiyo imesaidia kupandisha ufaulu na kuwajengea uwezo, kuwaandaa Wanafunzi wenye madarasa.
Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa wamehamasisha jamii kuchangia chakula cha mchana huku akisema mitihani ilifanyika kulingana na ratiba iyoelekezwa.
Anaeleza kuwa Halmashauri iliendelea kuhamasisha wananchi kujitolea katika Ujenzi wa miundombinu ya shule pamoja na kuendelea kusimamia miradi inayotengewa fedha na Serikali kuu ili kupunguza uhaba wa miundombinu hiyo.
Pia Mkurugenzi huyo wa Mji Kondoa anasema Halmashauri hiyo imeendelea kutoa motisha kwa walimu na shule zinazofanya vizuri pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa walimu.
0 Comments