ASILIMIA 70 YA WAGONJWA WA SARATANI HUCHELEWA KUFIKA KWENYE VITUO VYA AFYA

 

📍Takwimu inaonesha saratani ya mlango wa kizazi inachanagia kwa asilimia 36 ya Saratani zote.

📍Asilimia 21 huchangia kwa vifo.

Na Asha Mwakyonde,DODOMA 

KAIMU Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Lotalis Gadau, amesema kuwa asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi huwasili katika vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa hatua ambayo tayari saratani hiyo imekwisha sambaa katika maeneo ya mwili.

Tanzania ni kati ya nchi zenye idadi kubwa ya wagonjwa saratani ya mlango wa kizazi barani Afrika na inakadiriwa takribani wanawake zaidi ya 10,241 wanapata saratani hiyo kila mwaka na 6,525 hupoteza maisha.

Hayo ameyasema leo Aprili 25,2025 Jijini Dodoma wakati akiwasilisha mada kuhusu saratani hiyo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Kitaifa 2025, yanafanyika mkoani Tabora kuaznia Aprili 24 hadi 30 mwaka huu, alisema kuwa takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha saratani hiyo inachanagia kwa asilimia 36 ya Saratani zote na asilimia 21 huchangia kwa vifo.

Meneja mpango huo ameongeza kuwa wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa kizazi hawapati huduma za ugunduzi wa haraka na batibabu sahihi.

Akizungumzia dalili za saratani hiyo haina dalili na hugundulikwa kwa kuchunguzwa na wataalamu wa afya huku ameeleza kuwa dalili za baadae ni kutokwa na uchafu, damu kwenye uke ,kupata hedhi bila mpangilio maalum.

"Dalili nyingine za baadae ni kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ngono, kupata maumivu makali wakati wa kujamiana ," amesema Gadau.

Aidha ameihamasisha jamii na kuikumbusha kupitia vyombo vya habari umuhimu wa kupima afya zao hasa Saratani ya mlango wa Kizazi kwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 14 na kwenda kupata Chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa watoto wenye umri kuanzia miaka 9 hadi 14.

Awali Afisa Programu Elimu kwa Umma kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk.Tumaini Haonga amesema kuwa serikali kupitia Wizara ya afya imeendelea na mkakati wa kuhakikisha utoaji wa huduma za chanjo unafikiwa kwa kiwango kikubwa ambapo utoaji huduma hiyo umefikiwa kwa wastani wa Kitaifa wa zaidi ya asilimia 95 kwa walengwa mbalimbali.

Amesema mikakati waliyonayo katika utoaji wa huduma za chanjo ni pamoja na kuwa na Vituo 8500 vinavyomilikiwa na Serikali na Taasisi binafsi na kuendeleza huduma Mkoba na Tembezi kuanzia ngazi ya jamii na Mashuleni ili kuwafikia walengwa husika pale wanapopatikana. 

"Tanzania imeendelea kuwa na mafanikio makubwa katika utoaji huduma za chanjo na vituo hivi 8,500 vinatoa huduma bure kwa walengwa," ameeleza Dk.Haonga.

Dk.Haonga ameongeza kuwa wana walengwa wachache ambao hawafanikiwi kupewa chanjo na ni wale baadhi ambao hawajapata kabisa kutoakana sababu mbalimbali na wengine ni lile kundi ambalo limepata sehemu ya dozi ya chanjo kwa zile dozi zinazotolewa kuanzia mbili.

Post a Comment

0 Comments

WAZIRI MHAGAMA AWATAKA WATENDAJI KUSIMAMIA SHERIA ZA AFYA APASAVYO