TASAC YAONGEZA USALAMA WA VYOMBO VYA USAFIRI MAJINI KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kwa kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri wa majini kwa kuhakikisha vinatoa huduma salama na ufanisi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo yote ya mwambao na maziwa.

Hayo yalisemwa leo Juni 17,2025 jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alipotembelea banda la TASAC katika maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yenye Kaulimbiu isemayo "Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji" amesema hatua zinazochukuliwa na shirika hilo katika kusimamia ubora wa vyombo vya majini ni muhimu kwa maisha ya watu na uchumi wa taifa.

Waziri huyo ameeleza kuwa ni jambo la kutia moyo kuona TASAC inachukua hatua za makusudi kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo baharini na kwenye maziwa.

"Nimefurahishwa sana na kazi mnazozifanya napongeza juhudi zinazofanywa na TASAC kuhakikisha usafiri wa majini umeimarika ," amesema Simbachawene.

Kwa upande wake, Afisa Msajili na Mkaguzi Mkuu wa Vyombo vya Usafiri Majini kutoka TASAC, Mhandisi Saidi Mkwawa amesema kuwa wanaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki na watengenezaji wa vyombo vya usafiri majini ili kuhakikisha vinajengwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Ameongeza kuwa wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo yote ya mwambao na maziwa kwa lengo la kudhibiti ubora na kuhakikisha huduma salama kwa watumiaji.

 "Shirika limeweka mkazo mkubwa katika ukaguzi wa vyombo vya majini amesema Mhandisi Mkwawa.

Naye Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TASAC, Amina Miruko ameeleza kuwa Shirika limejipanga kuhakikisha huduma za usafiri majini nchini zinaendeshwa kwa viwango vya hali ya juu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma kuhusu umuhimu wa utii wa sheria na kanuni zilizopo.

Amefafanua kuwa kwa sasa wameimarisha udhibiti wa shughuli zote za usafiri majini ili kulinda maisha ya wananchi, mali zao na pia kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia usafirishaji wa majini.

Miruko ameongeza kuwa TASAC imeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya uwakala wa meli (Sura ya 415), na ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mwaka 2018.

Afisa huyo ameyataja baadhi ya majukumu ya shirika hilo kuwa ni pamoja na kusimamia sekta ya usafiri wa majini, kuratibu biashara ya usafirishaji wa majini, pamoja na kutoa huduma za uwakala wa meli.

Hatua zinazochukuliwa na TASAC, katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ili kuboresha usalama na ufanisi wa vyombo vya usafiri majini nchini.

Post a Comment

0 Comments

UTALII NA MADINI ZINACHANGIA KWA PAMOJA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA