Na Anangisye Mwateba, Dodoma
SERIKALI imesema sekta ya madini na utalii ni nguzo muhimu zinazotegemeana katika kukuza uchumi wa Tanzania, kutokana na mchango wake katika kuvutia wawekezaji, kuongeza ajira, na kuimarisha mapato ya taifa.
Akizungumza wakati wa kufunga Jukwaa la Uziduaji 2025 lililofanyika jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, amesema kuwa kupitia minada na maonesho ya madini yanayofanyika nchini, watalii na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi huvutiwa kuja kujifunza namna biashara ya madini inavyofanyika, kushiriki katika shughuli hizo na pia kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
“Tunaona jinsi sekta ya madini inavyochangia kwa kiasi kikubwa katika kuvutia watalii, kukuza huduma za malazi, ukarimu na hata kuongeza uelewa wa mila, desturi na tamaduni za Watanzania kwa wageni wanaotembelea nchi yetu,” amdsema Mhe. Kitandula.
Aidha, ametaja changamoto zinazojitokeza katika shughuli za uchimbaji madini, hasa kwa wachimbaji wadogo, kuwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti usio na mpango.
Amesisitiza kuwa ni lazima kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.
“Hatupaswi kuacha changamoto hizi zikiendelea. Tunahitaji kuhakikisha kwamba uchimbaji wa madini unakuwa na manufaa ya kweli kwa jamii na taifa kwa ujumla, lakini pia unazingatia uhifadhi wa mazingira,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Mhe. Kitandula, majadiliano yaliyofanyika katika jukwaa hilo ni chachu ya maendeleo ya sekta ya uziduaji na yamelenga kuhakikisha kuwa sekta hiyo inatoa mchango mkubwa zaidi katika ustawi wa taifa kupitia usimamizi bora, uwazi, na ushirikiano wa pande zote muhimu.
0 Comments