DCEA: MKONO WA CHUMA KUWAFIKIA WAUZA DAWA ZA KULEVYA


Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam 

KAMISHNA Jenerali kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo 

amesema wale wote wanaendelea kufanya biashara ya dawa za kulevya mkono wa chuma utawafikia, pumzi ya moto itawaelekea na watakaoendelea kufanya biashara hiyo, kukaidi maelekezo ya serikali watahakikisha kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa na watakamata na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria.

Pia amesema kuwa wale wote ambao wataendelea kutangaza,kusifia kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya iwe ni kwa mavazi, nyimbo kwa jambo lolote ambalo linaonesha anasifia, kuhamasisha hatua ya sheria itaendelea kuchukuliwa.

Hayo ameyasema leo Julai 5, 2025, alipotembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba' amesema kuwa ndani ya vifungu vya sheria hususani kifungu Namba 24 ambacho kinasema yoyote anaye hamasisha matumizi ya dawa za kulevya anachukuliwa hatua kama wahalifu wengine.

Kamishna Jenerali huyo amewaomba Watanzania kuachana matumizi ya dawa za kulevya, usambazaji pamoja na kuzalishaza wa dawa hizo.

Akizungumzia hali ya dawa za kulevya nchini kwa sasa ameeleza inaendelea kuwa nzuri, kuimarika kutokana na oparesheni mbalimbali ambazo wameendelea kuzifanya.

"Hadi sasa suala la Heroini, Methamphetamine, kokeini limeadimika, zimepungua kwa kiasi kikubwa huku akisema kwenye vijiwe hakuna tena waraibu.

Amefafanua kuwa hiyo inatokana na serikali baada ya kuwachukua waraibu ambao wameathiriwa na na kuwapeleka katika vituo vya tiba ambapo wanapata matibabu bure na wanaendelea kuimarika na kurudi katika hali zao za kawaida.

Kamishna Jeneral huyo ameeleza kuwa kwa sasa wapo katika oparesheni maalum ya kuhakikisha wanatoa elimu katika nchi nzima kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo Vikuu.

"Tuna fanya oparesheni ya kuwakamata wale wote wanaojihusisha na biashara ya usambazaji,uuzaji na uzalishaji wa dawa za kulevya lengo ni kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi tunamaliza kabisa tatizo la dawa hizi nchini na wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na suala la dawa hizi," amesema.

Aidha amesema kuwa wale ambao bado hawajajiingiza katika dawa za kulevya na wale ambao tayari wameshaingia kwenye dawa hizo waweze kujua vituo vya kutoa huduma.

Kamishna Jenerali huyo amesema kuwa serikali inatoa huduma za matibabu bure kwa wale wote ambao tayari wameathuriwa na dawa hizo.

Lyimo amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita ina hakikisha wananchi wote wanarudi kwenye mfumo,afya njema ili kuungana kwa pamoja kujenga uchumi wa nchi.

"Mamalaka ya kupambana na dawa za kulevya ipo katika maonesho haya na kwamba tuna mabanda mawili tukianzia na hili hapa na lile lilopo katika banda jumuishi katika ofisi ya Waziri Mkuu," amesema.

Ameongeza kuwa lengo la kushiriki katika maonesho hayo ni kuwapa wananchi elimu ili wajue aina za dawa za kulevya wajue pia wanakamatwa na dawa hizo wajue sheria inasemaje.

Amewataka Wazazi kuhakikisha kuwalinda watoto wao wasijingize kwenye matumizi ili kuhakikisha wanajenga kizazi imara na uchumi endelevu wa nchi.

Post a Comment

0 Comments

DCEA: MKONO WA CHUMA KUWAFIKIA WAUZA DAWA ZA KULEVYA