Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Uwakala wa meli Tanzania(TASAC), Nahodha Musa Mandia amesema usalama wa bahari kwa kiasi kikubwa umeimarika na kwamba matukio ya maharamia yameisha.
Hayo yameyasemwa leo Julai 5, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TASAC kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba'
alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinafanyakazi kubwa kuhakikisha usalama katika bahari unaendelea kuimarika hivyo tunavipongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Amesema usafiri wa bahari umezidi kuimarika kiulinzi na usalama hali iliyopelekea kuendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini.
"Natia rai kwa wananchi kutembelea kwenye banda letu lililopo katika maonesho haya ya sabasaba ili waweze kujifunza namna shirika linavyofanya kazi katika kuhakikisha linalinda usalama katika bahari," amesema.
Ameongeza kuwa wapo katika maonesho hayo kwa ajili ya kuelimisha watu kujua ni kiasi gani usafiri wa bahari unachangia katika uchumi wa nchi.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa uwepo wa mazingira mazuri katika bahari umepelekea utalii kwa njia ya bahari unakua lakini pia miradi ya mafuta na gesi inaimarika.
Aidha aliwataka wananchi kutembelea banda hilo kwa lengo la kupata elimu ili kufahamu shughuli zinazofanywa na Shirika hilo.
0 Comments