Na Asha Mwakyonde,Dar es Salaam
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeanza rasmi kutoa mafunzo ya urubani kwa vitendo ambapo vijana 10 wa Kitanzania wamejiunga, wakiwemo wanawake wanne na wanaume sita.
Ada ya mafunzo hayo ya urubani hapa nchini ni shilingi milioni 34 wakati mwanafunzi akienda kusoma nje ya nchi atalipia zaidi ya shilingi milioni 200 kwa mafunzo hayo hayo.
Akizungumza Julai 8,2025 jijini hapa katika banda la NIT kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Mkufunzi wa Urubani kutoka chuo hicho, Ashrafa Ramadhan, alisema kuwa chuo hicho kina vifaa vya kisasa na wataalamu waliobobea katika nyanja hiyo.
Mkufunzi huyo amesema kuwa wamejipanga vizuri kuanzia hatua za awali za kufundisha ardhini hadi mafunzo ya angani.
“Mimi ni miongoni mwa wakufunzi kumi waliopo, na tumeshaanza rasmi mafunzo ya urubani chuoni kwetu Nawakaribisha vijana kufika kwenye banda letu wapate elimu ya kina kuhusu kozi ya urubani," ameeleza.
Ameongeza kuwa NIT imewekeza katika miundombinu na teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo bora ya kitaalamu na ya kimataifa huku gharama zikiwa nafuu ikilinganishwa na vyuo vya nje ya nchi.
Mkufunzi ambaye ni rubani ameeleza kuwa sifa za kujiunga na mafunzo hayo ni kuwa na elimu ya angalau kidato cha nne, na umri wa kuanzia miaka 17.
Hata hivyo, ameeleza kuwa suala la afya, hasa uwezo wa kuona rangi kwa usahihi, ni jambo linalopewa kipaumbele kikubwa kwa wanaotaka kuwa marubani.
“Mara nyingi watu huwa wanahoji kama tumejiandaa vya kutosha, napenda kuwaondoa hofu. Tumejipanga ipasavyo.Tuna vifaa vya kisasa vya kufundishia marubani kabla hawajapanda ndege, na ndege mpya kwa ajili ya mafunzo zipo tayari,” amesisitiza.
Aidha ametoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo adhimu ya mafunzo ambayo yana nafasi kubwa ya ajira na ujasiriamali katika sekta ya usafiri wa anga.
Amewataka Wazazi kuwaunga mkono watoto wao kuingia kwenye fani hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wageni hapa nchini.
NIT kimekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya usafirishaji, na kuanzishwa kwa kozi ya urubani ni hatua nyingine muhimu katika kujenga uwezo wa ndani wa wataalamu wa anga nchini.


 
 
 
 
 
0 Comments