Na Asha Mwakyonde,DAR
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),Charles Sangweni, ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi ya kimkakati.
Pia ameeleza kuwa PURA inajivunia utekelezaji wa agenda ya Nishati Safi ya kupikia iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa imeanza kutekelezwa kwa vitendo na kuonyesha mafanikio makubwa.
Hayo ameyasema leo Julai 9,2025 katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba' alipotembelea banda la mamlaka hiyo amesema PURA itaendelea kuhakikisha kila hatua ya maendeleo inawagusa Watanzania moja kwa moja.
Amesema mwitikio wa wananchi kuhusu nishati safi umekuwa mkubwa, na kwamba mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha haina mwanya wa kumuangusha Rais katika agenda hiyo muhimu ya kitaifa.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa PURA wanaitekeleza agenda hiyo kikamilifu huku akisema katika maonesho haya wameona mwamko mkubwa wa wananchi katika masuala ya nishati safi ya kupikia na kwamba hiyo inaonyesha uelewa unaongezeka.
Akizungumzia nafasi ya Watanzania katika sekta ya mafuta na gesi, Sangweni amesema tangu kuanzishwa kwa PURA, kumekuwa na ongezeko kubwa la ushiriki wa Watanzania, ambapo kwa sasa asilimia 85 ya ajira katika sekta hiyo zinashikiliwa na wazawa, ikilinganishwa na chini ya asilimia 55 hapo awali.
0 Comments