Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geophrey Pinda alifafanua jambo wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Kuhende akitoa taarifa wakati wa kikao cha Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Baadhi ya washiriki wa Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali wakimsikiliza Naibu Waziri wa katiba na Sheria Geophrey Pinda ( hayupo pichani),wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi hiyo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geophrey Pinda ( Wa nne kutoka kushoto kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari waliohudhuria kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
SERIKALI ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuondoa uzembe na vitendo vyote vya rushwa na ubadilifu mahali pa kazi ikiwa ni pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija katika utekelezaji wake na kwamba ni wajibu wa Kila mtumishi wa serikali kuhakikisha anatimiza majulumu yake.
Pia ofisi zote za Umma zimetakiwa kutekeleza masharti ya kisheria kwa kuunda mabaraza ya wafanyakazi na kufanya vikao ipasavyo ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Hayo yamesemwa jijini hapa Machi 8, 2022, na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geophrey Pinda wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali cha mwaka 2021 na 2022, Pinda amesema mchango wa Ofisi hiyo ni kusimamia haki za watu kwa misingi sahihi.
Amesema kuwa mabaraza ya wafanyakazi yalianzishwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri serikali katika ngazi, Idara, taasisi na wizara kuhusu usimamizi wa kazi na rasimali watu majukumu, kulinda haki na wajibu kwa ajili ya wafanyakazi,kujenga hali bora za wafanyakazi, kuhusu maslahi yao na kusimamia ustawi katika sehemu za kazi.
"Namshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha ofisi hii muhimu ili liweze kutekeleza majukumu yake kisheria ipasavyo ya kuiwakilisha serikali na taasisi zake katika mashuri ya madai na usuluhishi ndani na nje ya nchi. Natambua tangu kuanzishwa kwa ofisi hii maalumu mashauri ya serikali na taasisi zake na maslahi mengine yameendelea kusimamiwa ipasavyo katika vyombo vya utoaji haki," amesema Naibu Waziri Pinda.
Aidha ameipongeza ofisi hiyo ya Wakili Mkuu wa serikali kwa kufanya kikao hicho ikiwa ni utekelezwaji wa matakwa ya sheria kwa Kila ofisi ya Umma kuwa na Baraza la Wafanyakazi pamoja na kufanya vikao kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri hiyo ameongeza kwamba ni matumaini yake kuwa kupitia Baraza hilo ambalo ni kiunganishi kati ya Menejimenti na wafanyakazi wa ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali na watumishi wataendelea kushirikiana katika mambo yenye tija.
Amesema Baraza hilo halipaswi kuangalia masuala ya wafanyakazi bali kujadili na kuangalia mwelekeo wa serikali na nafasi ya Wakili Mkuu wa serikali katika kufikia malengo yake.
Ameeleza kuwa utaratibu wa mabaraza ya wafanyakazi unalenga kukuza uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi mbalimbali ili mfanyakazi anapotekeleza majukumu yake awe anafahamu mikakati wa miaka mitano ijayo ya ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali, mpango wa mwaka wa fedha na namna ya kutekeleza.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa serikali Boniface Kuhende ameeleza kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi kwa kushirikiana kutatua migogoro inayohusu serikali pamoja na washiriki wake, wananchi na serikali ili kuharakisha maendeleo.
"Ofisi hiyo inatumia njia ya usuluhishi, majadiliano na kufungua kesi mahakamani na mashauri hayo huisha kwa wakati na hurejesha amani kwa upande husika na kufanya kuendelea na shughuli za maendeleo," amesema.
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2020 na 2021 hadi kufikia Machi 2022 aambapo wameazimisha mwaka mmoja wa Rais Samia ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali imeweza kupata mafanikio mbalimbali.
Ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuongezewa baheti kutoka bilioni 11.4 kwa mwaka wa fedha 2020 2021 hadi bilioni 12. 13 kwa mwaka wa fedha 2021 hadi 2022 sawa na ongezeko la asilimia 5.4.
0 Comments