Meneja wa Mradi wa Kuunganisha Mfumo wa Gesi Asili katika Magari (CNG), Dkt. Esebi Nyari, akitoa maelezo ya ufungaji gesi kwa Naibu Waziri wa kilimo Antony Mavunde alipotembelea banda la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), imejivunia mafanikio makubwa katika eneo la uunganishaji wa mifumo ya gesi katika magari, ambapo tangu mwaka 2018 magari zaidi ya1,000 yanafanyakazi katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kutumia gesi asilia.
Meneja wa Mradi wa Kuunganisha Mfumo wa Gesi Asili katika Magari (CNG), Dkt. Esebi Nyari, aliyasema hayo katika mjadala ulioandaliwa na Watch Tanzania kuhusu mchakato wa uhamasishaji matumizi ya gesi asilia na umeme kama mbadala wa nishati ya mafuta kwenye magari ulioshirikisha wadau mbalimbali.
Dkt. Nyari amesema usalama wa mifumo hiyo ni mkubwa kutokana na ubora na uimara wa vifaa pamoja na ufungaji unaofanywa kitaalamu na kuwatoa hofu wamiliki wa magari ambao bado wana hofu na mfumo wa gesi wakihofia usalama ambapo amesema tangu DIT imeanza kuuganisha mfumo huo katika magari hakuna gari lililoleta shida kutokana na mfumo huo.
Ameongeza kuwa kwa kuwa gesi asilia inayotumika katika magari ipo kwenye mgandamizo mkubwa, ubora wa vifaa vyake pamoja na ufungaji wa mfumo mzima lazima uzingatiwe.
“Hatari kubwa ya mfumo wa gesi asilia ipo kwenye mtungi kule nyuma ambapo presha ni kubwa, katika kuhakikisha usalama, mitungi hii hufanyiwa majaribio mengi kama ya moto, risasi na presha ambayo yanafanywa na mtengenezaji wa mitungi husika kabla haijaingizwa sokoni,” anasema Dkt. Nyari.
Anasema usalama unazingatiwa pia katika ufungaji wa mitambo katika magari kwa kufungwa na watu wenye uzoefu na utaalamu wa kutosha kwa kufuata sheria ambapo kabla gari halijaingia barabarani lazima lipitie kwa mkaguzi ili kulikagua na kujiridhisha kuwa mifumo hiyo imefungwa vizuri.
“Baada ya mkaguzi kujiridhisha kuwa mitambo hiyo imefungwa vizuri, huwa anatoa kibali ambacho kinamruhusu sasa mtumiaji kwenda kujaza gesi na kuendelea kulitumia, kwa sasa nchini tuna wakaguzi watano na wanalazimika kukagua magari yetu hapa DIT,” ameongeza Dkt. Nyari.
Kuhusu dhana ya baadhi ya watu wanaodai kuwa kuweka gari mfumo wa gesi asilia ni kuliharibu, Dkt. Nyeri anasema DIT inachofanya ni kuongeza mfumo wa gesi na sio kuingilia mfumo wa mafuta uliopo katika gari husika.
Amesema ili kuhakikisha kuwa utaalamu huo unakuzwa na kuenziwa, DIT na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wananaendelea kutoa mafunzo katika eneo la gesi na kuongeza kuwa wahitimu wana jukumu na nafasi ya kuhakikisha kuwa Tanzania inaelekea katika uchumi wa gesi kupitia matumizi ya gesi asilia katika magari na viwandani.
Aidha, amesema DIT ipo katika mchakato wa kuanzisha mafunzo ya muda mrefu katika eneo la kufunga mifumo ya gesi asilia katika magari na pia kuanzisha somo mahususi la kufunga mifumo hii katika magari.
Ameogeza kuwa, kwa muda mrefu kumekuwa na uhaba wa wakaguzi wa magari, lakini DIT kwa kushirikiana na wadau kama Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), UDSM na wadau wengine waliendesha mafunzo ya muda mfupi kwa kumtumia mtaalamu mmoja aliyekuwepo kutoa mafunzo na kufanikisha kuwapata wakaguzi watano waliopo nchini.
Ufungaji wa mfumo wa gesi kwenye magari ni mradi ambao uko chini ya Kampuni Tanzu ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT Co Ltd) ambayo ina jukumu la kuboresha bunifu mbalimbali zinazobuniwa ndani ya Taasisi hiyo na kuzipeleka sokoni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba anasema hamasa ya matumizi ya gesi asilia nchini imeongezeka huku akibainisha kuwa ubadilishaji wa mfumo wa magari ya mafuta kwenda katika mfumo wa gesi unaofanywa na DIT unakwenda vizuri.
Anasema kutokana na upandaji wa mafuta, watu wengi wameingia katika kubadilidha mifumo ya magari na kutumia gesi ambapo Kituo cha DIT kinachofanya kazi ya kubadilisha mifumo hiyo kimeripoti ongezeko la magari yaliyohitaji huduma hiyo ambayo imefikia 300 hadi 400 kwa mwezi.
“Idadi ya vituo vya kuweka mfumo wa gesi imefikia vitano na mazungumzo yanaendelea kuhakikisha kuwa vituo vya kujazia gesi vinajengwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, na baadaye kwenda mikoani ” anasema Mramba katika mjadala huo wa mtandaoni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Modestus Lumato alisema pamoja na kujivunia hamasa ya Watanzania kuchangamkia matumizi ya gesi badala ya mafuta, wataishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuviondolea kodi vifaa vya mfumo gesi kuondolewa kodi ili vipatikane kwa bei nafuu kuongeza hamasa wananchi kufunga mfumo wa gesi katika magari yao.
0 Comments