Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof. Kenneth Bengesi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Oktoba 25,2022 jijini Dodoma.
NA ASHA MWAKYONDE, DODOOMA
SERIKALI imejipanga kuongeza uzalishaji wa sukari kupitia viwanda vilivyopo ikiwemo kufanya upanuzi wa viwanda ili kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 380,000 hadi tani 671,000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Pia mikakati ya serikali Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msukumo mkubwa na mazingira mazuri katika kuhakikishakuhakikisha nchi inaondokana na tatizo la upungufu wa sukari.
Hayo yamesemwa Oktoba 25,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof. Kenneth Bengesi, wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2025/26, jumla ya uzalishaji wa sukari nchini utakuwa ni tani 756,000 ambapo watakuwa wamevuka lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) la kuzalisha tani 700,000.
Amesema kuwa watahakikisha miradi mipya ambayo ni Kiwanda cha Sukari Bagamoyo kimeshaanza na kwa msimu huu watazalisha tani 20,000 na mwaka 2023 wanatarajia kufikia tani 35,000 ambao ndio uwezo wa kiwanda kwa sasa.
"Kwa upande wa Kiwanda cha Mkulazi Morogoro wanatarajia kuanza uzalishaji wa sukari mwaka 2023, na pia wanatarajia kuzalisha hadi tani 50,000 ifikapo mwaka 2025/26," amesema.
Pia ameeleza kuwa kuendelea na uendelezaji wa teknolojia katika kilimo cha miwa, ambapo bodi kwa kushirikiana na TEMDO wanasaidia utengenezaji wa kiwanda kidogo, kipya cha sukari ambacho kitajengwa kwenye maeneo ambayo yana uwezo wa kuzalisha miwa michache isiyokidhi kuweka kiwanda kikubwa ambapo kwa sasa ujenzi wa kiwanda hicho kipo katika asilimia 75.
Tasnia ya sukari inachangia zaidi ya asilimia moja ya Pato la Taifa na imeweza kutengeneza ajira za moja kwa moja zaidi ya 24,000 na zisizokuwa za moja kwa moja zaidi ya 180,00.
0 Comments