Na WAF – DODOMA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya afya Dkt. John Jingu amewataka wataalam wa afya kuandaa mpango mkakati madhubuti utakaokua ni muongozo katika kutoa huduma za afya nchini na kuwafikia wananchi popote walipo ikiwemo kuangalia fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Dkt. Jingu amesema hayo leo wakati akifungua kikao cha Wataalam mbalimbali wa afya waliokutana jijini Dodoma kwa ajili ya kuandaa mpango wa Wizara ya Afya wa kuboresha utoaji wa huduma za nchini.
Dkt. Jingu amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na taasisi binafsi imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya hivyo anategemea uwekezaji huo ulete matokeo Chanya kwa nchi hivyo wataalam wanatakiwa kuchangamkia masoko ya ndani na nje.
“Rais Samia Suluhu Hassan anataka sekta ya afya ikue Tanzania na kutoa mchango mkubwa kuliko hivi sasa, haya yote yanawezekana kwa kuweka sera na miongozo mizuri lakini kutoa huduma kupitia taasisi zetu mbalimbali za umma na za sekta binafsi”. Amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa sekta ya afya kazi yake sio kutoa huduma peke yake kwa wagonjwa au kuzuia na kupambana na magonjwa bali inatakiwa iwe chanzo cha ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo amewataka wataalam hao kuweka mikakati itayofungua fursa za kiuchumi kupitia afua mbalimbali za afya.
“Mwelekeo wa Rais ni kuona huduma za afya hapa nchini zinakua ni nzuri lakini bidhaa za afya zikiwemo dawa, vifaa na vifaa tiba vinapatikana muda wote kwa urahisi na kwa bei ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kuimudu lakini pia muangalie vikwazo vinavyokwamisha fursa na muweke mikakati ya kutoa vikwazo hivyo ili nchi ipate masoko ya nje," amesema Dkt. Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu amesema kuna fursa nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki, kusini mwa jangwa la sahara, Afrika na duniani kwa ujumla kuhusu masuala ya afya akitolea mfano mkataba wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Bohari ya Dawa (MSD) kuhusu kununua, kuuza na kusambaza bidhaa za dawa kwenye nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa ni mojawapo ya fursa ya kiuchumi Tanzania inayonufaika nayo.
Amesema kupitia mikataba mbalimbali nchi iliyojiwekea inaweza kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo amewataka wataalam hao kujadili na kuandaa mkakati wa Wizara utakaokua ni chachu ya kusukuma ukuaji wa uchumi kwa kuchungulia fursa zilizopo.
0 Comments