MAAFISA WA BRELA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI

Dar es Salaam 

Maafisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara  na Kurugenzi ya Miliki Ubunifu wametakiwa kuzingatia maadili na kufanya kazi kwa weledi ili kufanikisha malengo waliyojiwekea.                                   

 Hayo yamesemwa katika mafunzo yanayoendelea katika ukumbi wa APC Bunju "A" Kinondoni, Jijini Dar es Salaam, ya kuwajengea uwezo maafisa hao kuhusu namna ya kuandaa mashauri ambayo BRELA inatakiwa kushiriki Mahakamani kutoa ushahidi wa kesi mbalimbali.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Jaji Mstaafu kutoka Mahakama  Kuu, Mhe. Jaji Robert Makaramba amewataka kuzingatia namna ya kuandaa mashauri na kujiepusha na vitendo ambavyo vitasababisha kesi mbalimbali kuchelewa.

Pia amewataka kutojihusisha na vitendo ambavyo vitasababisha kuhujumu mwenendo wa mashauri mbalimbali ambayo msingi wake ni kutoa haki, ambapo maafisa wa BRELA hushiriki katika kutoa ushahidi mbalimbali kwa kesi ambazo Taasisi huitwa mahakamani.

"Mnatakiwa kuzingatia namna ya kuandaa mashauri vizuri na vilevile baada ya kutoka katika kesi hizo, zikiwa bado hazijaamuliwa mjiepushe na kuyaongelea yanayoendelea Mahakamani ili kutohujumu mienendo ya kesi hizo", amesema Mhe. Jaji Makaramba.


Pia amewataka kuwa na ushirikiano na kuwa na hali ya kujifunza kila wakati ili kufahamu namna ya kuiwakilisha vyema Taasisi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza Septemba 20 na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 22, 2023, yanawahusisha moja kwa moja maafisa wanaotakiwa kushiriki katika mashauri mbalimbali Mahakamani kwa lengo la kuwajengea uwezo, na umakini  ili waweze kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU