WANANCHI WATAKIWA KUTOA USHAHIDI MAHAKAMANI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Richard Thadei Mchomvu akitoa ufafanuzi wa changamoto kwa wananchi wa shehia za Pangawe, Kinuni, Mwembe Majogoo na Mnarani Zanzibar.

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B" Mhe. Hamida Mussa Khamis akitoa elimu ya Kuzuia na kupambana na Uhalifu kwa wananchi wa Shehia za Kinuni, Pangawe, Mwembe majogoo na Mnarani Zanzibar.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mjini Magharibi ACP. Cleophance Magesa akitoa elimua ya Polisi Jamii kwa wananchi wa Shehia za Kinuni, Pangawe, Mwembe Majogoo na Mnarani

Mbunge wa Jimbo la pangawe Zanzibar Haji Amri Haji akihamasisha wananchi kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kupambana na uhalifu.

Na Saidi Malala,Zanzibar

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limesema wananchi kutohudhuria mahakamani kutoa ushahidi wa matukio mbalimbali ya kihalifu ni miongoni mwa sababu zinazopelekea vitendo vya kihalifu kuendelea kufanyika katika Mji wa Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Richard Thadei Mchomvu alipofanya kikao na wananchi wa shehia ya Kinuni,  Pangawe, Mnarani na Mwembe Majogoo zilizopo Wilaya ya Magharibi B" Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limeendelea kuweka mikakati thabiti ya kuzuia na kupambana na uhalifu na udhalilishaji ndani ya Mkoa kwa kuwashirikisha wananchi katika Ulinzi Shirikishi ili waweze kubaini na kutanzua changamoto za kihalifu katika maeneo yao lakini changamoto kubwa ni kutotoa ushahidi mahakamani.

" Kuna matukio kadhaa ya kihalifu yalitokea katika maeneo yenu, wananchi waliyaona na kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha watuhumiwa kituoni, hilo mnalifanya vizuri sana katika kupambana na uhalifu. Changamoto iliyopo ni kwamba mkifikisha watuhumiwa kituoni mnakuwa wagumu kwenda mahakamani kutoa ushahidi hivyo kupelekea kesi hizo kufutwa na wahalifu kurudi mitaani kuendelea na uhalifu" amesema Kamanda Mchomvu

Aidha Kamanda Mchomvu amekemea vikali baadhi ya wananchi kufuta kesi kwa kuogopa muhali katika jamii hali ambayo inawapa mwaya wahalifu kuendelea na vitendo hivyo.

"Hapa nina majalada ya kesi zilizofutwa ambazo wananchi wa maeneo haya ya Kinuni na Nyarugusu wamefuta kesi kwa kuogopa muhali. Kuna kijana hapa alishambuliwa na wahalifu saba (07) lakini mama mzazi wa kijana huyo akaamua kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwenda kufuta kesi ili wahalifu hao wote waendelee tu kufanya uhalifu" ameongeza ACP. Mchomvu.

Ameeleza kwamba baadhi ya  wananchi  huungana pamoja kwenda kumuomba Mlalamikaji ili kufuta kesi na asipofanya hivyo wanamtenga katika jamii jambo ambalo linaleta hofu kwa mlalamikaji hivyo kuamua kufuta kesi hizo na mhalifu kuendelea kufanya uhalifu mtaani.

" Wahalifu waliopo katika maeneo yetu ni zao la jamii yetu sisi wenyewe, hivyo kuendelea kuwalea na kuoneana muhali haiwezi kuwa kinga ya kumaliza uhalifu katika maeneo yetu, jamii lazima iamke na kuchukua hatua za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo"

Akijibu swali la mwananchi aliyeeleza kwamba baadhi ya Askari kutotoa huduma nzuri vituoni, Kamanda Mchomvu amesema katika Vituo vyote vya Polisi vina namba za simu za viongozi, hivyo amewataka wananchi kupiga simu kwa namba hizo pindi wanapokutana na huduma isiyoridhisha katika vituo hivyo ili hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka.

"Nawaomba wananchi mnipigie simu muda wowote mnapokutana na huduma isiyoridhisha kwenye vituo vya Polisi, pigeni ile namba iliyoandikwa RPC  inapatikana masaa 24 hata iwe saa nane Usiku nipigie nitakusaidieni" amesema Mchomvu.

Vilevile ametoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya uwepo wa usafiri katika vituo vya Polisi ambapo wananchi wamelalamika kuwa wanapowakata watuhumiwa kuna uchelewaji wa usafiri, Kamanda Mchomvu amesema Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi limeagiza magari na Pikipiki za kutosha ambazo zitakuja kumaliza kabisa changamoto ya usafiri vituoni.

"Kila Wilaya itapata magao wa magari na pikipiki kwahiyo changamoto ya usafiri katika vituo vya Polisi inakuja kuwa hadithi na sio changamoto tena"

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambae ni  Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B" Mhe: Hamida Mussa Khamis amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanya vikao vya kusikiliza changamoto za kiusalama katika maeneo ya Mkoa huo pamoja na kutoa elimu ya Polisi Jamii ambapo amesema kwa kiasi kikubwa inaleta matokeo chanya.

" Binafsi nikiri kwamba maeneo haya yana matukio mengi ya kihalifu, hivyo pamoja na vikao ambavyo naendelea kufanya katika shehia lakini nimpongeze Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi na timu yake kwa kuliona hili na kuamua kufanya vikao na wananchi wa ukanda huu" amesema Mhe. Hamida.

Aidha Mheshimiwa Hamida  amesema changamoto ya vikundi vya ulinzi shirikishi kutokuwa na ofisi, Serikali ameahidi kujenga Ofisi za Masheha ambapo katika mpango wa awamu ya kwanza zitajengwa ofisi 75, ambapo Wilaya ya Magharibi B" imepata nafasi ya kujengewa ofisi za Masheha na amefafanua kwamba ofisi hizo zitatumika pia na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi katika kutimiza majukumu yake.

Aidha amewataka masheha kufanya vikao vya mara kwa mara katika shehia zao ili kusikiliza changamoto zinazowakabiri wananchi na kuzichukulia hatua.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Cleophance Magesa amesema wazazi na walezi wanapaswa kuimarisha malezi bora ili kuwajenga watoto katika maadili mema.

"Kuna mamlaka nne zinapaswa kushiriki katika malezi ya watoto ambazo ni Familia, Jamii, mamlaka ya kidini na maskulini, hizi mamlaka zikitimiza vizuri wajibu wake basi tutarajie kuwa na jamii iliyo na maadili mema" alisema Magesa

Nae Mbunge wa Jimbo la Pangawe Mhe. Haji Amri Haji ameahidi kushirikiana na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Ali Suleiman Ameir ambae ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar katika kusikiliza kero za wananchi wa jimbo hilo na kuzifanyia kazi.

Nao wananchi wa shehia hizo wamepongeza juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuzuia na kupambana na uhalifu ambapo kipekee walimpongeza Mkuu wa Kituo cha Polisi Kijito Upele Mkaguzi wa Polisi (Inspector) Ali Issa pamoja Mkaguzi shehia wa Shehia ya Tomondo Mkaguzi Msaidizi (A/Inspector) Omar Khatib ambao wanafanya kazi bega kwa bega na vikundi vya Ulinzi Shirikishi vya maeneo hayo.

Kikao kama hicho kitafanyika tena baada ya miezi mitatu ili kufanya tathmini ya ushiriki wa wananchi katika kutoa ushahidi mahakamani ili kupambana na uhalifu.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU