WAZIRI MAVUNDE: TUTABORESHA TAFITI ZA GST, WACHIMBAJI WADOGO KUNUFAIKA

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

SERIKALI  kupitia Wizara ya Madini imesema kuwa itahakikisha ina boresha  shughuli za utafiti wa madini nchini zinazofanywa na  Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST),lengo likiwa ni kutoa taarifa sahihi za kijiolojia za madini ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo.

Pia  imeweka mikakati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuzalisha ajira kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo Septemba 11,2023 na 
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika kikao cha pamoja kati ya wachimbaji wadogo chini ya mwamvuli wa Shirikisho la Vyama vya wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), ameeleza kuwa  tafiti hizo zitasaidia kugundulika kwa madini ya kimkakati, malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea ambayo  itasababisha uwepo wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini pamoja na  kuzalisha ajira mpya katika Sekta hiyo.


Amesema kwa sasa wachimbaji wadogo wanakosa taarifa muhimu ya kujua wapi ni sehemu sahihi ya upatikanaji wa madini hali inayosababisha uwepo wa uwepo wa migogoro kwa wachimbaji hao.

"Ili kuongeza uwekezaji katika Sekta hii Wizara kupitia Taasisi ya GST imeweka mkakati wa kuhakikisha tafiti za kijiolojia zinafanyika katika maeneo yote nchini ifikapo mwaka 2030 ili kuwezesha wachimbaji kuendesha shughuli zao bila kubahatisha" amesema Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa mkakati huo utaupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini na wachimbaji wakubwa wa madini.


Naye, Rais FEMATA John Bina, amesema kuwa Mchango wa Wachimbaji Wadogo umefikia asilimia 40 katika Sekta ya Madini kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Madini kwa mwaka wa 2022/2023 ilinganishwa na mchango wa asilimia 8 tu ya mwaka 2016/2017.

"Tunaiomba  serikali kupunguza kodi katika mitambo inayoingizwa nchini ili kurahisisha shughuli za uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi," amesema

Rais huyo ameeleza kuwa wapo katika hatua za mwisho za  kuanzisha benki kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo nchini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO ).

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI