Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAANDISHI wa habari Jijini Dodoma wamepatiwa mafunzo ya ya namna ya kuripoti habari za kijinsia katika vyombo vya habari na jamii hasa kwenye masuala ya uongozi,urithi na mgawanyo wa mali kupitia mradi wa Advancing Gender Equality in Media and Civil Society.
Mafunzo hayo yameandaliwa
na Chuo Kikuu Cha Aga Khan kupitia mradi wa Shule ya mawasiliano ya vyombo vya habari ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (GSMC), (The Aga Khan University graduate school of media communication), iliyopo nchini Kenya ambao unatekelezwa katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza jijini Dodoma Oktoba 27,2023 Mratibu wa mafunzo hayo Pauline Muriuki ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ni kuleta usawa wa kijinsia kwa wanaume na wanawake katika vyombo vya habari na jamii hasa kwenye masuala ya uongozi,urithi na mgawanyo wa mali.
Ameongeza kuwa katika jamii hakuna usawa wa kijinsia huku akitolea mfano wa baadhi ya akina mama kudhulimiwa haki zao na wanaume pindi wanapoachana.
"Hata ikitokea nafasi mbalimbali za uongozi wanaume ndio wanaonufaika zaidi kuliko wanawake, hii ndio iliyotufanya tuje kutoa mafunzo hayo lengo ni kuwa na nafasi sawa katika jamii" amesema.
Pauline amefafanua kuwa waandishi wa habari ni watu wenye ushawishi katika jamii na kwamba wakielewa vizuri masuala ya kijinsia watakuwa ni watoa elimu kupitia kalamu zao.
0 Comments