Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo (kulia) wakimkabidhi cheti cha jina la Biashara Bi. Salima Mfinasoka (katikati) aliyekamilisha taratibu za usajili leo tarehe 26 Oktoba, 2023, katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), walipotembelea maonesho ya BRELA na wadau wake yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu Dar es salaam
MKUU wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa kwa kurasimisha biashara zao Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili kunufaika na biashara wanazozifanya.
Mhe. Mpogolo ametoa wito huo leo tarehe 26 Oktoba, 2023, alipotembelea Maonesho ya BRELA na wadau wake yanayofanyika katika uwanja wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mpogolo amesemal engo la maonesho ya BRELA ni kuhamasisha wadau kurasamisha biashara zao kwa wingi hasa kipindi hiki ambacho BRELA imeandaa maonesho na kuzishirikisha taasisi mbalimbali za Umma na kutoa huduma mahali pamoja.
Aidha Mhe. Mpogolo amefafanua kuwa mfanyabiashara anaporasimisha biashara yake hutambulika na taasisi za kifedha, humwezesha kupata zabuni mbalimbali pamoja na kuwa rasmi kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo ameipongeza BRELA kwa kuandaa Maonesho yenye tija kwa wafanyabiashara na kwa ukuaji wa uchumi nchi.
“Nimefurahishwa sana na huduma nzuri inayotolewa na BRELA, hivyo basi wafanyabiashara ambao bado hawajarasimisha biashara zao ni vyema wakafuata taratibu sahihi za kusajili”, amesema Mhe. Bulembo
Maonesho haya ya siku tano (5) ya BRELA na Wadau wake yenye Kauli Mbiu "Urasimishaji biashara katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda yalifunguliwa Oktoba 24, 2023 na yatahitimishwa Oktoba 27, 2023 Sambamba na Mkutano wa BRELA na Wadau wake utakaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
0 Comments