OFISI YA WAZIRI MKUU YAPONGEZWA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria kilichofanyika  Bungeni Jijini  Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga (Kulia) akiteta jambo na Kamishna Jenerali wa Mamlaka a Dawa za Kulevya Nchini Bw. Aretas James Lyimo, wakati wa kikao cha kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria kilichofanyika  Bungeni Jijini Dodoma.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyambo, akiongoza kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika, Bungeni Jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga, akiwasilisha Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa mwaka 2023/2024 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Bungeni Jijini Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu, Dodoma 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria, imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kwa kazi nzuri ya mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.

Pongezi hizo zimetolewa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakati wa  wasilisho la Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa mwaka 2023/2024  Bungeni  Jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho Mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Dkt Alice Kaijage amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutokana na uwepo wa  Mwongozo na mfumo wa Mawasiliano wa kubadilishana Taarifa akisema  kuwa mifumo inapelekea utendaji mzuri.

“Mifumo ni muhimu sana kwa kubadilishana taarifa na taasisi nyingine na zoezi zima la kutoa taarifa kupitia mawasiliano ya simu,” Amesema Mhe.Dkt. Alice.

Pia ameongeza kuwa uanzishwaji wa  vilabu vya wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari  vinavyotumika  kutoa ujumbe na mafunzo dhidi ya mapambano ya Rushwa na Dawa za Kulevya vimesaidia kujenga uelewa kwa wanafunzi kutambua mchango wao katika mapambano hayo pamoja na kufahamu madhara ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na hatua za kuchukua kuepuka ili kutimiza ndoto zao.

Aidha Aliipongeza Mamlaka hiyo kutumia vizuri fungu la fedha za maendeleo kwa kuanzisha nyumba za utengamao zinazosaidia warahibu kujifunza stadi mbalimbali zinazowasaidia kujiimarisha kiuchumi.

Akiwasilisha Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa mwaka 2023/2024 kwa kamati hiyo  Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema,  Mamlaka imetoa Elimu kwa Umma Kuhusu Madhara ya Dawa za Kulevya, mafunzo ya udhibiti wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa wadau na wataalam wa dawa tiba, maduka ya dawa, Asasi za Kiraia na vituo vya forodha.

Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri Nderiananga amebainisha kuwa  Mamlaka imetoa elimu kuhusu madhara ya kilimo cha bangi na mirungi katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha mazao hayo katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, na Mara, na kuongeza kuwa  Mamlaka ilitoa elimu juu ya madhara ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini.

 Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini Bw. Aretas James Lyimo, amesema tafiti zinaonesha kuwa uwepo wa  kundi kubwa la wanafunzi kujiingiza katika dawa za kulevya hali iliyosababisha  Mamlaka hiyo kuweka nguvu kubwa katika vilabu shuleni.

“Kutokana na utafiti uliofanyika kutuonesha uwepo wa wanafunzi wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya tukaamua kuongeza nguvu shuleni kwa kuandaa  mwongozo wa vitabu shuleni na vyuoni unaohusisha Mamlaka ya Kuzuiya na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na Mamlaka ya Dawa za Kulevya na kufikisha elimu kwa wanafunzi wote kuhusiana na madhara ya dawa za kulevya,”Amefafanua Kamishna Jenerali huyo.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU