HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA YAPATA HATI SAFI 2022/2023


Mbeya 

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imepata hati safi katika Hesabu za Serikali zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.

Hayo yamesemwa na Mstahiki meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mhe. Dormohamed Issa Rahmat katika kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Mbeya kilichoketi leo tarehe 30/4/2024 katika ukumbi wa Meya uliopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Mstahiki Meya Dormohamed amesema Halmashauri imepata hati safi kutokana na ushirikiano mkubwa ulipo baina ya waheshimiwa madiwani na wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambao kwa pamoja wamefanya kazi nzuri ya usimamizi wa miradi na matumizi mazuri ya fedha za Serikali, huku akiipongeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi mzuri na ushauri wanaoendelea kuutoa ndani ya Halmashauri.

“Nichukue nafasi hii niwapongeze wakuu wa idara na vitengo, watumishi pamoja na waheshimiwa madiwani wote kwa kuliheshimisha jiji la Mbeya na ndiyo maana tumepata hati safi hongereni sana”, ameeleza Mhe. Meya.

Aidha Mhe. Meya amesema ni wakati mzuri sasa kwa Waheshimiwa Madiwani kuendelea kusimamia miradi mbalimbali inayopelekwa kwenye maeneo yao, ili thamani ya fedha ya miradi hiyo iweze kuonekana sambamba na kuwataka wataalamu wa jiji la Mbeya kuwafahamisha madiwani wote miradi inayokwenda kwenye Kata zao.

“Tumeletewa Milioni Mia Nane (800,000,00/=) na Serikali ya Mama Samia kwa jitihada kubwa za Mbunge wetu Dkt. Tulia Ackson kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharula litakalogharimu kiasi cha shilingi 400,000,000, ujenzi wa jengo la wodi ya wakina mama litakalogharimu kiasi cha shilingi 200,000,000 pamoja na shilingi 200,000,000 zitakazojenga jengo la wodi ya wakina baba”,amefafanua Mhe. Meya.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Bw. John John Nchimbi ameelezea namna anavyoshirikiana vizuri na watumishi walio chini yake kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Halmashauri na anaamini mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 mambo yatakuwa vizuri zaidi.

Mkurugenzi Nchimbi ameeleza kuwa Halmashauri imepata kiasi cha Shilingi Bilioni Moja na Milioni Miatano(1,500,000,000) ambazo zitatumika kukarabati madarasa katika shule zote zilizochakaa za Halmashauri ya Jiji la Mbeya na takribani madarasa mia tatu (300) yatakwenda kukarabatiwa ili ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha ujao wa 2024/2025 angalau kila Kata iwe imefikiwa katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya Bw. Edward Malima anayeshughulikia Serikali za Mitaa ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kupata hati safi na kumshukuru Mhe. Meya kwa kuongoza vizuri Baraza la Madiwani mpaka kuwezesha kupata hati hiyo, aidha ameiomba Halmashauri iendelee kushikamana ili hati safi ziwe na muendelezo na hiyo italetwa na mshikamano na umoja( Teamwork).

Aidha Bw. Malima ameliomba Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanyia kazi yale ambayo CAG ameyabainisha katika ripoti yake ili kukidhi matakwa ya kisheria lakini pia kuyatekeleza na kuyafanyia kazi maelekezo yote ya kamati ya Bunge (LAAC), huku akipongeza hatua iliyofikiwa na Halmashauri ya ukusanyaji wa Mapato wa asilimia 87.

Kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya Bw. Azizi Fakii,viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya Bw. Humphrey Msomba.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI