MAVUNDE: ASILIMIA 9.1 YA PATO LA TAIFA INATOKA SEKTA YA MADINI

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

BUNGE limepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kiasi cha shilingi bilioni 231.98 ambapo kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 140,661,200,000.00 sawa na asilimia 60.63 ni kwaajili ya miradi ya maendeleo mbalimbali na shilingi bilioni 91.3 ni kwaajili ya mishahara na matumizi ya kawaida. 

Mchango wa sekta ya Madini kwenye pato la taifa umezidi kuongezeka hadi kufikia asilimia 9.1 kwa mwaka 2023/24 ikilinganishwa na asilimia 7.2 kwa mwaka 2022/2022.

Akiwasilisha hutuba yake ya makadirio,mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 leo Aprili 30,2024 bungeni Jijini Dodoma Waziri wa madini Anthony Mavunde amesema mwenendo wa mapato ya fedha za kigeni kupitia Sekta ya Madini umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka.

Amesema mwaka 2023 madini yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3,551.4 yaliuzwa nje ya nchi sawa na asilimia 56.2 ya mauzo ya bidhaa zisizo za asili (non traditional goods) ikilinganishwa na mauzo ya dola za Marekani milioni 3,395.3 sawa na asilimia 56.0 mwaka 2022. Hivyo, mauzo ya madini ya mwaka 2023 yaliongezeka kwa dola za Marekani milioni 156.1 ambayo ni asilimia 4.6 kutoka mauzo ya mwaka 2022.

Waziri Mavunde amesema kwa upande wa madini ya almasi, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024,mwenendo wa biashara ya madini hayo duniani umeendelea kusuasua kutokana na mdororo wa uchumi uliosababishwa na madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine. 

Ameeleza kuwa madini hayo yameshuka bei duniani kwa asilimia 19 kwa mwezi Machi, 2024 na kwamba wastani wa mauzo ya madini ya almasi katika kipindi husika ni karati 201.71 

yenye thamani ya dola za Marekani 43,231,183.71 ikilinganishwa na karati 271.74 yenye thamani ya dola za Marekani 50,824,739.77 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023.

" Hatua zilizoanza kuchukuliwa na wazalishaji mbalimbali wa almasi duniani ni kupunguza uzalishaji wa almasi ili kuimarisha bei ya madini hayo," amesema Waziri huyo.

Akizungumzia Utekelezaji wa Shughuli Mahsusi amesema kuwa ili kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua na kuwanufaisha watanzania ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa,mwaka 2023/2024 Wizara ilijielekeza katika utekelezaji washughuli mbalimbali ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa. 

"Shughuli zingine ni pamoja na kuendeleza madini muhimu na madini mkakati,kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo,kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini,kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini na uanzishwaji wa minada na

maonesho ya madini ya vito na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,"amesema Waziri huyo.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU